Tuesday, August 3, 2010

Ukristo Korokoroni-Tanzania Usiyoijua!

Wapendwa hivi karibuni nilipata fursa ya kwenda kufanya kazi sehemu za Pemba katika shughuli zangu za ajira. Nilipokuwa nikielekea huko nilipata mashaka kama huko ninaweza nikapata kanisa la wasabato la kuabudia hivyo nilifanya mawasiliano na baadhi ya watu walio Unguja na wakaniambia kanisa lipo na kupewa mawasiliano.

Nilipofika Pemba nilifanikiwa kufika katika eneo wafanyalo ibada waadventista wasabato katika eneo la Chakechake maeneo yaitwayo vitongoji. Eneo hilo ni eneo la kambi ya jeshi ambapo ndipo jamii za kikristo zimepata fursa za kujenga maeneo yao ya ibada, na kwa upande wa wasabato wao wanatumia jengo la shule ya msingi ya zamani ya jeshi kufanyia ibada zao. Eneo hili ndilo eneo pekee ambalo waadventista wasabato wanakusanyika rasmi kufanya ibada kama kanisa. Nilipofika hapo nilikuta jamii iliyochangamka yenye kumtukuza Mungu huku watu wengi wakiwa wamewahi kuanzia darasa la walimu la saa 2. Kuwahi kwao ni kana kwamba kila mtu alitambua kwamba yeye ni muhimu na kuchelewa kwake kuna nafasi ya kuathiri mwenendo mziwa wa kanisa, kwani kanisa lina idadi ya jumla ya watu kati ya 20 ikijumuisha wakubwa na wadogo. Nilifurahishwa na vipindi vyao vilivyozingatia muda vyema.

Nikiwa ninasali katika kanisa hili ndipo nilipopata taarifa kutoka kwa mmoja wa wainjilisti wetu (ambaye ndiye aliyenielekeza kanisa kwa njia ya simu) kuwa eneo analoishi yeye halina uhuru wa kuabudu kama huo niliokuta hapo au ambao nimeuzoea mahali pengine popote. Jambo hili liliibua udadisi wangu na akanikaribisha kwenda kuabudu nao katika maeneo yao, mkoa wa kusini, wilaya ya Mkoani. Nilipanga na nilikwenda huko. Nilipofika huko nilistaajabia kukuta hali ambayo nilikuwa nafikiri inafanyika pengine nchi za uarabuni na kikomunisti ikiwa ipo Tanzania hii. Waumini wetu huko wanaabudu kwa kificho kikubwa.

Katika mazingira hayo jamii ya wenyeji nao kwa uaminifu katika imani yao wanafanya kila jitihada kuhakikisha ukristo haupenyi wala kupata nafasi katika jamii yao. Hivyo mtu yeyote anayebainika kuwa anajishughulisha na mambo ya dini ya kikristo huwa katika hatari ya kutopata nyumba ya kupanga, kutoungwa mkono katika shughuli zake za kiuchumi endapo kama zitawategea wao kwa kiasi fulani, mfano biashara. Kwa kuwa jamii kubwa ya waumini wetu walioko huko ni watu walioenda kujishughulisha na shughuli za kilimo basi hiyo huhatarisha upataji wao wa vibarua, makazi n.k. Kwa upande mwingine kwa wale walio tayari kukana imani wao huweza kupata vibarua vingi, makazi ya bure, na hata binti wa kuoa endapo watakuwa tayari. Hizi ni baadhi ya picha zikionyesha hali katika maeneo hayo ya ndugu zetu.



Ibada ya sabato ndani ya chumba kilichofungwa. Ibada hizi hufanyika bila hata ya uimbaji kuondoa hali ya kubainika. Ibada hizi huwa za muda mfupi tu kama nusu saa hivi. Wanaoonekana ni watu wote katika ibada hiyo (ongeza na mpiga picha)



Mwinjilisti (mwenye kofia gotini) akiwa na baadhi ya waumini na wanafunzi wa biblia muda wa alasiri siku ya sabato alipowatembelea kwa ajili ya kufanya nao ibada na kujifunza nao biblia. Hiyo nyumba ni nyumba ambayo haitumiki hivyo ilifaa kwa kujibanzia. Shauku ya neno ni kubwa sana katika maeneo haya.




Waumini pia hugawana maeneo na mwinjilisti kwa ajili ya kuwatembelea waumini ili kuwatia moyo na kujifunza nao. Waumini hao nao hualika marafaiki zao ili waweze kujifunza nao habari njema. Maeneo haya hayana wainjilisti wa vitabu, maduka ya ABCs- Adventist Book Centes. Vijuzuu pia havipatikani kirahisi



Picha ya pamoja mwinjilisti na waumini na wanafunzi wa biblia. Biblia hizi mwinjilisti hutembea nazo maana waumini hawa ni wapya na hawana biblia, hali kadhalika wanafunzi mara kadhaa humpasa kuwaachia biblia hizo ili wajifunze nazo.



Picha ya pamoja na waumini na wanafunzi wengine baada ya kufanya ibada ya jioni ya sabato ndani ya jiko lao.

Katika makambi yaliyopita mwezu huu wa 7 roho mpya 5 zilibatizwa kutoka maeneo haya. Binafsi niliguswa na mazingira haya na kuamua kufanya kitu kwa ajili ya ndugu zetu hawa katika Bwana. Unapokuwa unasali kumbuka watu hawa waishio katika mazingira magumu ya ibada na endapo ukiwiwa kufanya jambo kwa ajili yao unaweza kuwasiliana moja kwa moja na mwinjilisti wao kwa nambari 0718-109936. Pamoja na hayo kama kuna namna ambayo unaweza ukafikiria kuwa endapo ikibuniwa au ikitumiwa katika mazingira hayo inaweza kufaa kuwasaidia watu hawa wa Mungu katika kumwabudu Mungu wao usisite kutoa maoni yako. Kumbuka watu hawa wengi wao hawana miongozo ya kujifunza biblia-lesoni, hawana masomo ya nchi za mbali na hata mahala rasmi pa kuabudia, hivyo kufanya ibada zao kutokuwa kama zenye mfumo tuliuzoea bali zenye kuendana na mazingira, ambapo mara nyingine zisifanyike kabisa. Hivyo maoni yako yanaweza yakafanya jambo jema katika jamii hii ya kanisa la Mungu ulimwenguni.

9 comments:

  1. Rubara, nimelengwalengwa na machozi kwa sababu ya taarifa hiyo. Asante kwa kutupa mwanga wa hali halisi ilivyo Pemba."Baba Mungu tupe hekima ya namna ya kuendesha kazi katika maeneo kama haya.Baba wape neema waumini wapya katika sehemu kama hizi. Baba wape neema ya ziada wainjilisti wa maeneo kama haya. Baba lipe kanisa njozi bora hasa viongozi wetu wa kanisa katika namna ya kuhudumia wainjilisti na waumini katika maeneo kama haya. Amina!"
    R.D.Zembazemba

    ReplyDelete
  2. Ndg yangu Rubara, nimewiwa sana na kazi ya Bwana inayoendelea hapo visiwani ingawa katika hali ngumu kupita kiasi, lakini Bwana ataonyesha njia mateso yote haya yote yanamwisho wake, nimewasiliana na mwiinjilisti kama ulivyotoa namba yake na amesema ana mahitaji makubwa, tumuombe Mungu atupe moyo wa kutoa na jina lake litabalikiwa.

    Pia nikuombe uendelee kutpa lolote linalojili huko visiwani, Bwana awape nguvu na kazi yake itendeke

    Kayaga Nyachaga

    ReplyDelete
  3. Mtiwa mafuta wa Bwana, Mungu na awatie nguvu na huwezi jua mtu wa baba kwa nini umepewa nafasi ya kwenda kufanya kazi pemba, huenda ikawa Mungu alikutuma huko kwa makusudi maalumu. Basi uwe jasiri kama Joshua na kaleb, taarifa hizi zitatutia hamasa ya kufanya kazi wa hari na shauku kubwa ila baba arudi na twende nyumabani kwa baba. "THINK TWICE WHY GOD POSTED YOU THERE BRO"
    Chaulo, Jefta

    ReplyDelete
  4. Rubara, nashukuru sana kwa ujumbe huu unaogusa moyoni. Kwa ujumla nimepata ujuzi kama huo wakati nilikwenda unguja kwa mara ya kwanza Decemba 1996, nilikuwa unguja hadi 1997 kufanya kazi huko kama mwalimu wa sekondari. Wakati huo huko nako hali ilikuwa ngumu ingawa wasabato walikuwa na hospitali maeneo ya magomeni (nadhani) na kanisa maeneo ya Mombasa. Nakumbuka mwaka huo kulikuwa na matukio kadhaa ya hujuma dhidi ya makanisa ya madhehebu mbalimbali.. nakumbuka makanisa zaidi ya mawili yalichomwa moto kwa chuki ya kidini.. hata kebehi za wazi wazi agnainst christians... shida ya kupata nyumba ya kupanga.. kazini nakumbuka tulikuwa wakristo 3 tu kati ya staff ya watu 30 hivi.. nashukuru sana nilipokewa na kukaa kwa nyumba ya Mchungaji kwa mwezi mzima kabla sijapata mahali kupanga. Namkumbuka Mzee Biseko naye alinitia moyo sana..Kila sabato ilikuwa raha sana kukutana na wapendwa.. nadhani katika maeneo yenye dhiki ndipo imani inakuwa kubwa zaidi kuliko wakati wa amani.. maana nakumbuka tulikuwa na maombi sana ya usiku wa manane.. kuombea watu wa Bwana visiwani..nimetembelea Pemba pia kwa wiki kadhaa kikazi mwaka 2003.. unalosema Rubara ni hakika.. tena wakati huo tension za kisiasa zilikuwa zimeshamiri.. hivyo mtu wa Bara tena mkristo ulionekana kama msaliti fulani hivi..

    Wakati wa Ramnadhani ilikuwa ni haramu kula hadharani.. unaweza kukamatwa na kuchapwa viboko... natumaini unguja kumetulia kidogo hasa kwa kuwa na international interactions.. Kuna mengi ya kushuhudia ila tukiwa na wakati ninaweza kuwaeleza jinsi vijana wachache wa kisabato visiwani hasa unguja walivyojitoa kwa kazi ya Bwana mbali na magumu yote hayo...ni funzo kwetu tulio ha uhuru wa kuabudu. Masozi Nyirenda

    ReplyDelete
  5. Mungu akubariki kwa taarifa hiyo. Kwa baadhi yetu ni vigumu kuamini hayo ni mazingira yaliyopo Tanzania. Ni wakati wa kufikiria nini cha kufanya kwa ajili ya Ndugu hawa. Likini zaidi ni kuwaombea waumini hao na jamii inayowazunguka mbele za Mungu. GOD WILL MAKE A WAY!!! E. Mgata

    ReplyDelete
  6. OOOOOHHHH, is this Tanzania?????? MUNGU ATUTIE NGUVU NA MUUJIZA UTENDEKE TUPELKE INJILI HUKO, BE BLESED MAN OF GOD FOR SUCH A HEART TOUCHING MESSAGE

    ReplyDelete
  7. Tunaweza kufanya chochote jamani?? Hata waliotuletea ukristo hapa kwetu Africa walikutana na dhiki kubwa tu. Nasi tunaweza kufanya chochote kile kuwasaidia hawa ndugu waishie huko Pemba

    ReplyDelete
  8. Ubarikiwe mtumishi kwa kazi nzuri unayofanya. Mungu akutie nguvu unapowatia nguvu hao watiwamafuta wa BWANA.
    Neema Opiyo

    ReplyDelete
  9. aise yesu hajarudi bado kwa stailihii tufike huko hata kwa maombi na fedha kama sio wenyewe

    ReplyDelete