Sunday, April 26, 2009

Lesoni Somo la 5:- Ufunuo

(Warumi 1, Waebrania 1 & 4, Yohana 16)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani, Kihispania, Kizulu, nk.

Utangulizi: Je, inaleta mantiki kwamba kitu chochote kile hata kama ni chenye mkanganyiko na kigumu kuelewa kama ulimwengu, au hata yenye mkanganyiko na ngumu kuelewa kama jinsi ulivyo, ya kwamba vilitokea kwa bahati? Je, haileti mantiki zaidi kuamini kwamba magari ya kifahari yanayojulikana kama “Jaguars” yanaungwa/yanatengenezwa na sokwe (ambao ni wanyama), basi kuamini kuwa ulimwengu ulitokea kwa bahati? Maswali yenye mantiki zaidi ni haya: Ni Mungu wa aina gani tuliye naye? Je, ameamua kuzungumza na wanadamu na kuwaelezea kumhusu yeye mwenyewe? Je, twawezaje kupata ujumbe wake? Hebu tuingie kwenye kujifunza Biblia na kuona kile inachofunua juu ya haya maswali yote!


I. Baadhi ya Vitu vi Dhahiri!

A. Soma Warumi 1:18-19. Popote pale fungu linapoanza na “ghadhabu ya Mungu” huwa hujikuta ninakwepa! Kwa uhakika, Mungu anasikitishwa juu ya nini hapa? (Mungu anawakasirikia wale wanaouficha ukweli wake. Paulo aweza kuwa anasema mojawapo ya vitu viwili: 1) Waovu wanamkana Mungu kwa sababu matendo yao maovu yana kawaida ya kuuficha ukweli juu ya Mungu; au, 2) Wale wanaoukana uwepo wa Mungu hufanya hivyo kwa sababu ni waovu).

B. Soma Warumi 1:20. Kwa hakika ni kwa nini waovu hawako sahihi juu ya Mungu? (Uwepo wa Mungu ni wa dhahiri kutokana na kile alichokiumba).

1. Je, unakubali ya kwamba uumbaji humfunua Mungu? (Sabato iliyopita niliona sinema nzuri ajabu juu ya suala hili. Msemaji ni Louis Giglio na sinema hiyo inaitwa “Jinsi Mungu Wetu Alivyo Mkuu.” Unaweza kutizama sehemu ya kwanza ya sehemu kadhaa kwenye tovuti ya YouTube: http://www.youtube.com/watch?v=_82lZ2PpYQE&feature=related

2. Tambua Paulo anasema pia kuwa “hata wasiwe na udhuru”. Udhuru wa nini? Kumwamini Mungu, au kuamini kwamba Mungu ana ujumbe kwa ajili yetu? Nukuu ya Paulo kwa “asili ya kimbingu” ya Mungu inajenga hoja kuwa uasili huwasilisha baadhi ya ujumbe sahihi).

C. Soma Warumi 1:21-23. Ni ujumbe gani wa kwanza sahihi tunaoweza kujifunza kutokana na uumbaji? (Kwamba kwa kuwa kuna Mungu Muumbaji, inabidi tumtukuze na kumshukuru kwa uumbaji. Kutokana na hilo basi katika tafakari ya kawaida kinachofuata ni kwamba tusiabudu sanamu ya kitu kilichoumbwa, bali tumwabudu Muumbaji mwenyewe).

D. Hebu turuke mafungu kadhaa kwenye ujengaji hoja wa Paulo kuona ni jinsi gani zaidi anatumia wazo hili. Soma Warumi 1:26-27. Paulo anamaanisha nini anaposema “mahusiano ya asili?” (Kile kinachomaanishwa na asili ya vile tulivyoumbwa).

1. Ni jinsi gani uumbaji unatufundisha kuwa ushoga ni kosa? (Nilisikiliza ombi la fedha lenye hisia kali kwa ajili ya kurekebisha mazingira ili kwamba wale dubu wanaopatikana kwenye maeneo ya barafu wasiweze kupotea duniani. Naweza kubashiri, kwa akili ya kawaida, kwamba mojawapo ya masuala ya “kimazingira” ni kuwaambia hao dubu wasijihusishe na ushoga. Kwa hakika, wale waliokuwa wakiomba fedha hawakuwa na kitu kama hicho akilini. Lakini, naamini unaelewa dhana ya Paulo ya “mahusiano ya asili”.


II. Wasemaji!

A. Soma Waebrania 1:1. Fungu hili lasema kuwa Mungu anawasilianaje na wanadamu?

1. Hebu tizama mbadilishano huu. Paulo anatuambia tuangalie na kupata ujumbe kutoka kwa Mungu. Waebrania inatuambia kuwa Mungu aliongea nasi kupitia kwa manabii. Hoja ya uumbaji ni dhahiri. Ni sababu gani iliyo “dhahiri” tuliyonayo kuamini kuwa manabii walikuwa wakiongea kwa niaba ya Mungu? (Vitu viwili. Kwanza, kama uumbaji ni uthibitisho wa Muumba, je, siyo mantiki kwamba Muumba angetaka kuongea nasi? Pili, ujumbe wa manabii una mwelekeo ule ule. Kundi la watu wenye kujikweza nafsi katika karne kadhaa kwa uongo walidai kuongea kwa niaba ya Mungu, ungewatarajia kuwa na ujumbe mwingi kwa kadri ambavyo wajumbe wangekuwepo. Ujumbe wa moja kwa moja na usiobadilika unapendekeza kuwa umetoka kwenye chanzo kimoja).

B. Soma Waebrania 1:2-3. Kwa nini tuamini ya kwamba Yesu ni Mungu? (Kwanza, Yesu alidai kuwa ni Mungu (Mathayo 26:63-64; Yohana 12:44-46). Pili, ufufuo wake ulikuwa si kama kitu chochote kile kilicho ndani ya uwezo au mamlaka. Hili kwa hakika ni suala la “Mungu”.

1. Ni ujumbe gani kutoka kwa Mungu tulioupokea kupitia kwa Yesu? (Yesu anasema kuwa kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba yangu. Yohana 8:19. Kama tukijifunza maisha ya Yesu, tunaelewa asili ya Mungu.


III. Hebu Litazame!

A. Soma Waebrania 4:12-13. Wangapi kati yenu mnaweza kuelezea Biblia katika nyumba zenu kama “kitu kilicho hai na chenye nguvu” kinyume na “wazoa taka?”

1. Hebu tazama lugha iliyotumika “tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo”. Mada yetu inahusu kama kweli Mungu hujifunua kwetu. Ni jukumu gani linapendekezwa kuwa linafanywa na Biblia katika ufunuo huu? (Sisi sote tuna mawazo na makusudio ya moyo [mitizamo] ya jinsi gani inatupasa kuishi na kuwajali wengine. Biblia hujaribisha/huthibitisha mawazo haya na mitizamo hii dhidi ya viwango vya mwenendo wa Mungu).

2. Umewahi kusema kuwa “Natamani kwamba Mungu angefunua mapenzi yake kwangu” kwa chochote kile ukitamanicho kwa wakati huo?

a. Kama jibu lako ni “Ndiyo” je, umetizama kile Mungu alichokisema kuhusu mada hii kutoka kwenye maandiko ya Biblia? Kama jibu ni hapana, je, ulihitaji kweli kujua/kufahamu mapenzi ya Mungu?

B. Soma 2 Timotheo 3:16-17. Chanzo cha Biblia ni nini? (Mungu).

1. Biblia inaweza kuchukua jukumu gani katika kufunua mapenzi ya Mungu maishani mwetu? (Maneno “mafundisho, maonyo, kuongoza na kuadibisha” yanaonekana kujumuisha nyanja zote za maisha).


IV. Sikiliza!

A. Soma Yohana 16:7-9. “Msaidizi” ni nani? (Roho Mtakatifu).

1. Je, Richard Dawkins (mtu asiyemwamini Mungu) naye anasumbuliwa kidhamira kuhusu dhambi zake? (Tambua ya kwamba fungu la 9 linasema kuwa Roho Mtakatifu huwafanya kujisikia hatia hata wale wasioamini uwepo wa dhambi! (Au angalao basi hata wale wasiomwamini Yesu)).

B. Soma Yohana 16:10-11. Je, umewahi kujisikia hatia kwa dhambi hapo siku za nyuma? Umewahi kujisikia hatia siku za nyuma juu ya kile unachopaswa kukifanya kuhusu dhambi zako?

1. Kama umejibu “Ndiyo” kwa lolote kati ya hayo maswali mawili, je, huo ni uthibitisho wa ziada kuwa Mungu yupo na kwamba anajihusisha kwa dhati kabisa katika kuwasiliana na wanadamu?

2. Hili ni tatizo jingine linalowasumbua wale wanaoamini kuwa mwanadamu hakuumbwa bali alitokana na mabadiliko/mageuko ya pole pole kuanzia kwa mnyama. Kwa nini tukuze dhamira? Kwa nini hili “lundo la nyama” linaloendesha kazi za mwili liwe na mawazo yoyote zaidi ya kile ambacho ni muhimu kwa ajili ya kustahimilisha maisha?

a. Chanzo cha dhamira ni nini? Kama hatukuikuza, basi ni lazima iakisi nguvu zilizo nje ya uwezo wa mwanadamu, sawa?

C. Soma 1 Timotheo 4:1-4. Je, twaweza kuwa na dhamira mbaya? Dhamira inayotuambia kuwa tusifanye vitu ambavyo vinakubalika kwa usahihi kabisa kufanya?

a. Je, wawezaje kutenganisha kati ya mawazo yako mwenyewe na ya Roho Mtakatifu anayenena nawe?

b. Je, wawezaje kutenganisha kati ya “roho wadanganyao na mambo yanayofundishwa na mapepo” na Roho Mtakatifu anayenena nawe?

D. Soma Mathayo 12:31-32. Kukufuru dhidi ya Roho Mtakatifu inamaanisha nini? Je, ina chochote cha kuhusianisha na kukanganya ujumbe wa Roho Mtakatifu na jinsi unavyofikiri wewe binafsi au inakanganya na majaribu ya kimapepo? (Ili kusaidia kubaini hili, tunahitaji kuangalia kuanzia kwenye msingi).

E. Soma Mathayo 12:22-24. Yesu alikuwa anaonyesha nini pale aliporejea juu ya kuongea dhidi ya Roho Mtakatifu? (Yesu anawaonya wale wanaohusianisha kazi ya Roho Mtakatifu na kazi ya Shetani.

1. Kwa nini hii iwe dhambi isiyosamehewa? Kwa nini kusema mambo mabaya kwa upande mmoja wa Utatu Mtakatifu iwe mbaya zaidi kuliko kusema mambo mabaya juu ya upande mwingine wa Utatu Mtakatifu?

F. Soma 1 Samweli 3:12-14. Mungu anatoa ujumbe kupitia kwa Samweli kwa Kuhani Mkuu Eli kuhusu wana wake wa kiume, makuhani. Je, huu pia ni mfano mwingine wa dhambi isiyosamahewa? Kama ni hivyo, je, kuna dhambi ngapi zisizosameheka zilizopo? (Sidhani kama kuna dhambi iliyopo isiyosameheke kivile. Kumbuka ya kwamba wana wa Eli walikuwa na jukumu pamoja na kushughulikia hatua za kufuatwa kwa ajili ya msamaha wa dhambi pale hekaluni. Walikuwa wameshikilia mzani wa mchakato wa msamaha wa dhambi. Kwa kuwa walitumia vibaya mchakato huo, wasingeweza kusamehewa. Mtizamo huo huo ndio uliopo wa “kumsononesha” Roho Mtakatifu. Ni sehemu ya muhimu sana katika mchakato mzima wa msamaha wa dhambi-hututia nafsi zetu hatiani kuhusu dhambi zetu.

G. Soma Tito 1:15-16. Unapoharibu dhamira yako, je, wajipenyeza sehemu ambayo, kivitendo, dhambi yako haiwezi kusamehewa kwa sababu umeharibu mchakato mzima?

H. Baada ya kuwa tumesema kwamba tunaweza kuharibu kazi ya Roho Mtakatifu, hebu turejelee kwenye suala letu ambalo hatukufikia muafaka wa jinsi gani tunaweza kutofautisha kati ya ujumbe wa Roho Mtakatifu unaotujia kupitia kwenye dhamira zetu na ujumbe mwingineo. (Soma tena Yohana 16:15. Roho Mtakatifu huchukua ujumbe wake kutoka kwa Mungu. Kwa hiyo, Ujumbe wa Roho Mtakatifu ni lazima uwe sawa na ujumbe mwingineo unaofunuliwa kutoka kwa Mungu-kupitia kwenye maandiko ya Biblia, manabii wa kweli na asili).

I. Kiwango chako cha tahadhari kwenye ujumbe wa Roho Mtakatifu kipo vipi? Unaweza kusikia sawia? Au ujumbe huwa umekuwa barely discernable?

J. Rafiki, tunaye Mungu anayehitaji kuwasilisha mapenzi yake kwetu. Je, utaambatana na ujumbe wake na kuhuisha maisha yako kufuatana na ujumbe huo? Je, utamsikiliza Roho Mtakatifu na kuwa tayari na muwazi kwa mwongozo wake?


V. Wiki Ijayo: Dhambi.

Somo hili limefasiriwa na kuandaliwa na
Mgune Masatu.

Wednesday, April 22, 2009

Lesoni Somo la 4: Uzima

(Yohana 10, Matendo 27 & 28, Luka 12)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani, Kihispania, Kizulu, nk.

Utangulizi: Je, umewahi kutafakari juu ya maisha yako? Yana mwelekeo gani? Ungependa yawe na mwelekeo gani? Pamoja na kazi zetu, luninga, mtandao, watoto, kazi za nyumbani, na utume/ujumbe, ni rahisi kujishughulisha na “masuala ya haraka” kwa muda wa siku nzima. Tupatapo muda wa kupumzika, tunautumia kwenye kitu kingine zaidi ya kukaa na kutafakari tu. Huenda tafakari ni kitu kinachofananishwa na yoga tu, kwa jinsi tunavyojihusisha, na si sehemu ya maisha yetu. Hebu tuchukue wasaa na kutafakari, kupitia kwenye maaandiko ya Biblia, kile inachomaanisha kuishi. Hebu na tuangalie malengo aliyonayo Mungu kwa ajili yako!


I. Kipofu na Anayeona

A. Katika Yohana 9, Yesu anamponya kipofu. Hiyo iliamsha mtafaruku kwa viongozi wa dini. Hebu tuangalie kisa hicho mwishoni mwa Yohana 9. Soma Yohana 9:39-41. Yesu anasema kuwa amekuja ulimwenguni humu kwa hukumu. Je, Yesu alikuja ulimwenguni kutuhukumu? (Soma Yohana 3:17-18. Yesu alikuja kuuokoa ulimwengu).

1. Kama Yesu hakuja kuuhukumu ulimwengu, je, ni aina gani ya hukumu ambayo Yesu anaiongelea katika Yohana 9:39? (Tunajua ya kwamba Yesu alikuja kufa kwa ajili ya dhambi zetu. Kwa hiyo, hukumu ni lazima, angalao kwa kiwango fulani iwe juu yake).

2. Ni aina gani ya hukumu itakayofanya vipofu waone na wale wanaoona kuwa vipofu? (Mungu aliye na nia ya kutuponya, Mungu aliye na nia ya kufa kwa ajili yetu, Mungu ambaye anaonyesha huruma kwetu hufungua macho yetu kuhusu asili ya Mungu. Mwovu ambaye analeta upofu, na anayejeruhi na kuua, Mungu hufungua macho yetu kuhusu asili ya pambano kati ya wema na uovu).

3. Ikiwa sasa tumeshamwona Yesu, je, tunahitajika kufanya nini? (Yesu anafundisha kwamba mara tunapoelewa masuala ya kiroho, basi tuna uamuzi wa kufanya ili kuzuia hatia- na hukumu).

B. Soma Yohana 10:1-2. Kama ningekuwa natizama kwenye nyumba ya jirani yangu, na nikaona mtu fulani akiingia kwenye nyumba hiyo kupitia dirisha lililo nyuma ya nyumba, je, nifikirie juu ya kitu gani? (Huyu ni mtu asiye na ufunguo. Huyu ni mtu asiye na mamlaka husika).

1. Ni nini malengo ya nyumba yenye mlango na kitasa? Lengo la zizi la kondoo na lango ni nini? (Ni kulinda viumbe vinavyoishi humo, kuhifadhi watu wanaohusika ndani na wasiohusika nje).

1. Je, hili lina uhusiano gani na mazungumzo ya Yesu juu ya upofu? (Yesu anasema kuwa Mafarisayo ni vipofu-au angalao basi wanatenda/wanajifanya kuwa wao ni vipofu. Yesu anatuambia kuwa kuna ukweli ulio dhahiri katika maisha-kama vile ukweli kuhusu milango-kwa wale walio na nia ya kutizama).

A. Soma Yohana 10:3-6. Je, u mbele ya wanafunzi wa Yesu kimtizamo hapa? Naelewa kile ambacho Yesu anasema kuhusu zizi la kondoo-ambacho tunaweza kulinganisha na majumbani mwetu-lakini je, tunalitumia vipi hili katika maisha yetu? (Hebu tuendelee kusoma).

B. Soma Yohana 10:7. Sasa tunaelekea pahala fulani. Kama Yesu ndiye lango, je, zizi ni nini na kondoo ni akina nani? (Nadhani sisi ndio kondoo. Zizi lazima liwe ulinzi wa maisha yetu. Yesu huruhusu watu sahihi kuingia zizini na kuwaweka wasiostahili nje ya zizi.

C. Soma Yohana 10:8-9. Wawezaje kulitumia hili maishani? (Kama Yesu ndiye lango la kuingilia lililoidhinishwa, na malango mengine yote ya kuingilia yanatumiwa na watu wenye kuleta madhara, hii humaanisha kwamba Yesu ana njia za kulinda na kuwezesha/kufanikisha maisha yetu. Ni kama nyumba salama iliyo na lango la kuingilia linaloangaliwa/lindwa.

D. Soma Yohana 10:10. Kama ningesema kuwa ningeweza kukupatia “maisha kamili,” ungeelewa kuwa hiyo inamaanisha nini?

1. Yesu amekuwa akiongea nasi kuhusu njia na ulinzi, je, maisha kamili yanahusianaje na hilo? (Kama unaishi maisha sawasawa na mafundisho ya Mungu (Yeye ndiye lango pekee kwa kile unachokiruhusu kupita kupitia kwenye lango hilo) una maisha yaliyo makamilifu).

a. Je, hii ni kweli? Kuna kila aina ya programu za kwenye luninga zinazonifundisha kwamba maisha makamilifu na yenye furaha yanahusisha vitu vingine zaidi ya vile vilivyvothibitishwa na Mungu. Je, kuna ukweli mwingine?

b. Ni nini juu ya watu ambao wanaamua kwamba wataishi kama vile wanavyotaka sasa na watamrudia Mungu baadaye? Je, kuna ukweli wowote juu ya hilo?

E. Soma Yohana 10:11-13. Kwa nini mtu anayelipwa/aliyeajiriwa hafanyi kazi nzuri? Je, sisi sote si “waajiriwa” pale inapokuja kwenye kazi zetu? (Walioajiriwa huangalia vitu kimantiki-kupoteza maisha yake hakuwezi linganishwa na mshahara wake. Kama akiyatoa maisha yake, atakuwa na kitu gani hapo sasa?).

1. Ni nini hoja ya Yesu kwa ajili ya maisha yetu? (Yesu hafanyi hili kwa ajili ya kupata pesa. Alionyesha kwamba alitujali kwa kuyatoa maisha yake kwa ajili yetu).

2. Hili lina nini cha kufanya nasi kuwa na wakati mzuri sasa kwa kutenda yale mambo ya kufurahisha tunayoyaona kwenye luninga? (Mambo “yote mazuri” yaonekanayo kwenye luninga huhusisha uajiriwa. Njia ya ulimwengu ni kuamua kile kilicho bora kwa “namba moja.” Misukumo inapokuja, wengine huishia kuumia/kupata mateso/mahangaiko.

3. Ni nini hoja ya msingi ya kiroho inayoweza kuonekana hapa? (Kama tutatizama, na kutokuwa vipofu, tutaona ya kwamba maelekezo ya Mungu kwa ajili ya maisha yetu yanabubujika kutoka kwenye upendo ulio mkubwa kiasi kwamba yu tayari kuyatoa maisha yake kwa ajili yetu. Hakuna hata mtu mmoja anayetoa “ukweli” unaodhihirishwa na programu ya luninga iliyo maarufu inajali kile kitakachotutokea. Wanajalisha juu ya kupata fedha kutokana na program hizo. Haijalishi ni masomo gani tunayojifunza kutokana na program hizo, hiyo siyo wajibu wao-walao hivyo ndivyo wanavyoliangalia suala hilo.

F. Soma Yohana 10:14-18. Je, Yesu analazimishwa kufa kwa ajili yetu? (Hapana! Tazama hoja ambayo Yesu anaifanya. Aliyatoa maisha yake kwa ajili yako. Kwa nini angekupa maelekezo ambayo yanaweza kukuangamiza? Maelekezo ambayo yangeweza kuwa na ukomo wa kuishi maisha makamilifu? Asingeweza. Lakini, mbwa mwitu na waajiriwa hawakujali. Sheria zao za kimaisha haziakisi hilo.

G. Kama ungeweza kutafakari kwa kitambo kifupi juu ya maisha yako na jinsi ambavyo ungeishi, je, uamuzi wako wa kichoyo ungekuwa upi? (Uamuzi wa kumfuata yule aliyekuwa na nia ya kufa kwa ajili yako! Kama ungetaka kufanya kile kilichokuwa bora kwa ajili yako, basi ungekataa ushauri wa wale ambao maslahi yao ni kwa ajili yao-siyo kwako.

1. Je, hitimisho hili lina ukomo kwa masuala ya kiroho? (Hapana! Yesu alitumia mpango-kutunza kondoo-kama mfano wake. Ushauri huu unahusika katika nyanja zote za maisha kama tutakavyoona katika sehemu inayofuata).


II. Maisha Yenye Ushawishi wa Kweli

A. Utakumbuka ya kwamba wakati Paulo alipokuwa akihubiri injili, alifungwa na alikata rufaa Roma. Akiwa kama mfungwa, aliwekwa kwenye mashua pamoja na kundi la wafungwa wengine wakielekea Roma.

B. Soma Matendo 27:10-12. “Nyanja zipi za ushawishi” zinahusishwa katika kisa hiki? (Tunaye Paulo anayemwakilisha Mungu na maslahi ya kiroho. Tunao wamiliki wa mashua wanaowakilisha maslahi ya kibiashara. Tunaye jemadari anayeiwakilisha Serikali.

1. Kama ungekuwa Paulo, na ungetaka maisha yako yawe na ushawishi kwenye biashara na Serikali ungedhani juu ya kitu gani kama kikwazo cha mafanikio katika wasaa huu? (Yeye ni mfungwa!).

a. Je, ushauri wa Paulo umezingatiwa? (Hapana).

C. Soma Matendo 27:14-20. Ni nini ambacho hakikufanya kazi kuhifadhi maslahi ya biashara na ya Serikali? (Nyenzo zao wenyewe).

D. Soma Matendo 27:21-26. Mungu anatendaje kazi kupitia kwa Paulo kushawishi biashara na Serikali? Je, ni kitu gani ambacho Paulo hakukifanya? (Paulo hakusema kuwa “Mungu ameleta hukumu kwenu”. Badala yake malaika alimjia Paulo na kumpa suluhisho la tatizo. Paulo alikumbushia biashara na Serikali ambapo hapo awali alikuwa amewapa ushauri sahihi).

1. Kama unataka kushawishi juu ya biashara na Serikali, je, unahitaji kuwa na silaha za aina gani? (Malaika za Mungu! Roho Mtakatifu. Udhibiti wa Mungu wa Matukio).

E. Soma Matendo 27: 30-32. Ni nani sasa anayeshikilia juu ya operesheni ya biashara na Serikali? (Mtu wa Mungu, Paulo).

1. Ilichukua muda gani kubadilisha hali ya kutofuata ushauri wa Paulo na kumfuata Paulo?

F. Soma Matendo 28: 1-4. Ni siku ya aina gani aliyonayo Paulo hapa? Ulimwengu unamwona Paulo kuwa ni mtu wa aina gani?

G. Soma Matendo 28:5-6. Ni nini mtazamo wa ulimwengu dhidi ya Paulo sasa? Ilichukua muda gani kufanya badiliko hili?

H. Soma Matendo 28:7-9. Paulo sasa anakumbana na Serikali ya Malta. Ni aina gani ya ushawishi ambao Paulo anaupa msukumo kwenye uongozi wa Serikali?

I. Ni somo gani ambalo kisa hiki kinatufundisha kuhusu kufuata sheria za Yesu tunapojihusianisha na biashara pamoja na Serikali?


III. Kutokuwa na Woga/Wasiwasi

A. Soma Luka 12:22-26. Angalia hususani fungu la 25. Jibu lake ni nini?

1. Ni vipi kama ningeuliza swali hilo tofauti: ni nani, kwa kudhibiti (mlo, uvutaji sigara, mazoezi, kuendesha gari, hasira) yake, anaweza kuongeza saa moja katika maisha yake? Ni wangapi kati yenu mngejibu “ndiyo” kwenye swali hilo?

a. Ni nini sasa, ulio muktadha wa kuishi maisha yasiyokuwa na wasiwasi? (Sidhani ya kwamba Yesu anatuambia twende tukalale chini ya madawati. Wakolosai 3:23-24 inapendekeza kinyume chake. Ufunguo wa maisha kamili na yasiyokuwa na wasiwasi unatokana na kufuata sheria za Mungu na kuacha mengine yote kwa Mungu).

B. Rafiki, chukulia jinsi ambavyo maisha yangekuwa kama ungeamua kuwa njia ya Mungu ndio mara zote ingekuwa ya kufurahisha kuliko kitu chochote, ya kupendeza zaidi ya chochote? Chukulia jinsi ambavyo maisha yako yangeweza kuwa na ushawishi wa juu kabisa kwenye biashara na Serikali. Kumtumikia Mungu kwa moyo wako wote ndio njia kuelekea kwenye maisha yasiyokuwa na woga/wasiwasi, maisha yenye mafanikio na ushawishi mkubwa! Je, utachagua njia ya Mungu leo?


IV. Wiki Ijayo: Ufunuo.

Thursday, April 16, 2009

Lesoni Somo la 3: Tumaini

(Zaburi 33, 39, 43, 71 & 146, 1 Petro 1)

Somo hili la lesoni limetafsiriwa kutoka Corp. 2009, Bruce N. Cameron J. D. Aidha, somo hili pia linaweza kupatikana kutoka www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza.

Utangulizi: Je unahisi matumaini yako yanapotea? Nilipokuwa katika umri wa miaka 20 na kitu niliamini kwamba Marekani ilikuwa ikielekea kwenye machweo. Kwa nini isiwe hivyo? Mataifa yote huinuka na kuanguka, kwa nini sisi isiwe hivyo? Kisha, Ronald. Reagan alichaguliwa rais na mtazamo wangu ulibadilishwa kabisa. Nikapata matumaini katika siku zijazo za Marekani. Sasa Marekani na dunia kwa ujumla yaonekana ya kwamba vinaingia (inaingia) katika nyakati ngumu. Je ni kwa jinsi gani mkristo atazame mambo haya? Wote twaishi katika nchi tofauti, je tumaini letu la siku zijazo linategemea matumaini ya mataifa yetu.
Hebu uwe mkweli na nafsi yako, je ungependa ukae katika giza, nyumba ya upweke, ukishikilia tumaini la kiroho tu? Hebu na tutazame katika mwanga wa Biblia na kuona aina gani ya tumaini Mungu huwapa wafuasi wake!


I. Tumaini au msaada?

A. Zaburi 146:5. endapo nikikupatia tumaini au msaada ni kipi utachagua?

1. Je hivyo viwili ni tofauti?

2. Ni kwa jinsi gani fungu hili linaonyesha kwamba viwili vyote hivi hufanya kazi pamoja? (Tumaini hilo katika Mungu hutupa msaada halisi.)

B. Soma Zaburi 146:6. kwa nini mtunga Zaburi anataja sifa za Mungu mara baada ya kuzungumzia wale ambao tumaini na msaada wao ni katika Mungu? (Hii huthibitsha kuwa Mungu anaweza kutenda. Kama Mungu anaweza kuumba mbingu na nchi, anaweza kutatua matatizo yako madogo!)

C. Soma Zaburi 146:7. tazama sentensi ya kwanza. Ni kwa jinsi gani sehemu ya kwanza ya fungu hili ni tofauti na sehemu ya mwisho wa fungu hilo? (Mungu anatoa haki na anatoa chakula!)


1. Ni kwa jinsi gani Mungu analifanya hilo? (Hili huenda likahusisha msaada wako)
2. Baada ya kunithibitishia haki, na sasa natambua ya kuwa Mungu anawaachia wafungwa! Je, haki hiyo ikoje? (Kiashirio ni kwamba walifungwa kimakosa. Mungu hutoa haki halisi katikati ya uonevu wa mwanadamu.)

D. Soma 146:8. Je wafikiri tunazungumzia wale ambao ni vipofu haswa? (Twafahamu ya kwamba Yesu alimponya kipofu (Mathayo 9:27-30), lakini uzungumziaji wa wale “walioinama” hunifanya niamini ya kuwa fungu hili linazungumzia pia wale ambao mizigo yao ni mizito. Hawa ni wale ambao wamekatishwa tamaa na mazingira kiasi kwamba hawawezi kuona tumaini lolote mbele yao).

1. Je, inamaanisha nini “kuona” masuala yajayo?

2. Je, ni kwa nini fungu linaongezea kuwa, jambo lenye kuonekana kama kutohusiana, kiashirio kwamba Mungu huwapenda wenye haki? (Mungu ana mvuto kwa wale wanaomheshimu. Utiifu husaidia ufahamu mzuri wa siku zijazo).

E. Soma Zaburi 146:9. Je, wajane, wasio washiriki na yatima wana kitu gani kwa ujumla? (Ni wale walio wanyonge katika jamii. Mungu ana mvuto kwa wanyonge na huingilia kati kuwasaidia dhidi ya waovu).


F. Je, ni tumaini la aina gani ambalo tunalipata kwenye haya mafungu kutoka Zaburi 146? (Tumaini la msaada wa dhati! Mungu anaweza kusaidia. Anasaidia kwa haki na kwa chakula. Anasaidia wenye msongo. Anawasaidia wale wasio na “nguvu” katika dunia hii. Anawatafuta wale wanaomtii).


II. Tumaini Makini

A. Soma Zaburi 33:18-19. Serikali huonekana kuweka vinyaka uso (kamera) nyingi ili kuweza kuchukua matukio ya wananchi wake. Je, unapendelea/unafurahia pale Serikali inapoweka “jicho lake” kwako? Na je, ni vipi kuhusu Mungu anapoweka jicho lake kwako?

1. Tulikuwa na marafiki waliokuwa na wana wa kiume watatu. Baba alikuwa nadhifu, lakini alikuwa mtu mwenye kuwa mbali kifikra. Mkewe anakumbuka jinsi jinsi alivyomuacha mumewe kwenye sehemu ya maduka makubwa “kumwangalia” mtoto wao mdogo kwenye kiti cha kusukuma. “Baba” akavutiwa na kitu kingine na hivyo akamwacha mtoto peke yake pale kwenye duka kubwa. Pale “mama” aliporudi na kumkuta mtoto peke yake pale madukani-kwa hakika kilikuwa kituko kilichosimuliwa mara nyingi! Je, ni nini kinachokujia/unachofikiria pale Mungu anapokuhakikishia kwamba anakuangalia? (Habari njema ni kwamba Mungu anafahamu kile ninachopitia. Anakuwepo pale ninapokumbana na matatizo na ananipenda).

B. Soma Zaburi 33:20-21. Kwa nini fungu linatumia neno “ngojea?” (Inaonyesha kwamba si mara zote Mungu anatekeleza ratiba zetu).

C. Soma Zaburi 33:22. Kwa nini unafikiri mtunga Zaburi anaelezea upendo wa Mungu kama “usioshindwa” katika muktadha huu? (Mungu ni msaada wetu na ngao yetu. Mara nyingine, yaweza kuonekana kuwa msaada na ngao havipo-hivyo kuwa sababu ya kungojea kwetu na tumaini letu. Mwandishi wa Zaburi anatuambia ya kwamba upendo wa Mungu haushindwi kutuhakikishia ya kwamba msaada unakuja).


III. Tumaini kwa Tabia Zetu

A. Soma Zaburi 39:7-8. nilipokuwa mdogo walimu wangu walinifundisha ya kwamba Mungu angenisamehe dhambi zangu, lakini ingenipasa kutaabikia matokeo ya dhambi. Ni tumaini la aina gani linaloongelewa katika mafungu haya?(Tunaweza kutumaini tu ya kwamba kiwango chetu kamili cha dhambi zetu hakitotufedhehesha. Mungu kwa ukarimu wake mara nyingine ametukinga dhidi ya matokeo kamili, yenye kufedhehesha ya dhambi zetu.)


B. Soma Zaburi 39:10-11. Je Mungu hutuepushia matokeo ya dhambi zetu? (Mungu huweza kutukinga dhidi ya kejeli za wadhambi wenzetu ikiwa ni matokeo ya dhambi zetu, lakini Mungu hutuadabisha kwa manufaa yetu wenyewe.)

IV. Tumaini katika hali yenye kukatisha tamaa

A. Soma Zaburi 43:5. Je waelewa ni nini mtunga Zaburi anasema? Je, umewahi kupitia nyakati ambapo moyo wako umenyong’onyea na unahisi na kukosa furaha na mwenye kusumbuliwa?
B. Ni nini tumaini letu katika nyakati hizo? (Ya kwamba Mungu atatuokoa katika kukata kwetu tama na huzuni zetu. Pengine huenda kumsifu Bwana ni mojawapo ya mwanzo wa suluhisho. Binafsi kumsifu Mungu huhuisha nafsi yangu.)


V. Tumaini katika umri mkubwa

A. Soma Zaburi 71:9. Je ni kwa jinsi gain tumaini hubadilika kwa kadiri uzee unapokuja?

1. Fikiria kwamba ungekuwa unategemea wengine kwa mahitaji yako mengi katika maisha yako. Ni kwa jinsi gani hiyo ingeathiri mtazamo wako?

B. Soma Zaburi 71:10-12. Inaonekana kwamba mfalme Daudi ndiyo mwandishi wa hili (komentari zinatofautiana katiaka jambo hili), na anahofu na maadui zake wa kisiasa. Je, inaweza kuwa hii ni hofu tu ya mfalme mzee, au inawezekana jambo hili linaweza kutokea hata kwa wafanyakazi wazee?
1. Je inawezekana jambo hili huambatana na umri mkubwa?
2. Je bado tuna tumaini hata katika umri mkubwa? Na ni nini ni tumaini letu? (tumaini letu lippo katika Bwana, na nia yake ya kutuokoa mapema.)


VI. Tumaini katika wokovu

A. Mpaka sasa tumekuwa tukijifunza nini Biblia kuhusu tumaini katika Bwana kwa msaada wa hakika na thabiti katika maisha yetu.

B. Soma Tito 1:1-3. ni nini tumaini la maisha yetu katika muktadha wa maisha yetu ya kikristo. (Ya kwamba tutapata uzima wa milele.)
1. Ni katika nini tumaini letu la maisha ya milele hujengwa? (Kabla ya mwanzo wa wakati Mungu aliweka ahadi kuwapa wanadamu maisha ya milele. Yesu alifaulu katika ahadi hiyo.)

C. Soma Petro 1:3-5. Mbali na uzima wa milele, ni tumaini gani lingine tulilo nalo kuhusu mbingu? (Ya kwamba kutakuwa na urithi usioharibika.)
1. Na kwa wakati uliopo nini kinaendelea kwetu? (1 Petro 1:5 hutuambia kwamba kupitia amani tunalindwa na nguvu za Mungu mpaka wokovu wetu ufike! Pamoja na matatizo tuliyonayo tuna tumaini la uzima wa milele.)


VII. Utukufu na tumaini

A. Tu wenye baraka kiasi gani! Tunaweza tukawa na tumaini katika Bwana kwa msaada kwa sasa na pia tuna tumaini kwa uzima wa milele wa utukufu. Hii yote huwezekana kupitia Yesu. Tufanye nini kwa sasa? (Soma 1 Yohana 3:2-3. tunajitakasa.)
1. Humaanisha nini sisi kujitakasa? Ni Mungu tu ndiye mtakatifu. (Tunapaswa kujibidisha, kwa uweza wa roho mtakatifu, kwa fikra sahihi na maisha sahihi.)

B. Rafiki habari gani kwako? Je unapitia matatizo katika maisha yako? Mungu anakupatia matumaini na msaada hapa duniani na sasa – katika ratiba yake, na si yako. Muhimu zaidi, Mungu hutupa tumaini kwa maisha ya milele. Je, unaishi kama mtu mwenye matumaini kwa Mungu?


VIII. Wiki ijayo: Uzima.


Somo hili limetafsiriwa na kuandaliwa na
Masatu Mgune

Sunday, April 12, 2009

Last Days Message



Beloved, Jesus is truly coming back soon!!
Enjoy the message from very humble lips.

Wednesday, April 8, 2009

Uchambuzi lesoni ya 2: Imani

Somo hili la lesoni limetafsiriwa kutoka Corp. 2009, Bruce N. Cameron J. D. Aidha, somo hili pia linaweza kupatikana kutoka www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza.

Somo la 2: Imani

Waebrania 11, Zaburi 19, Yohana 20, 1 Petro 1, Luka 8

Utangulizi: Tunaambiwa ya kwamba imani siyo ushawishi wa kimantiki. Je, unakubaliana na hili? Chukulia ya kwamba wanafunzi wa Yesu waliamini Yesu angerudi wakati wa uhai wao. (Tazama 1 Wathesalonike 4:15-18). Sasa ni takriban miaka 2,000 baadaye. Nimewasubiria watu ambao wamekuwa wakichelewa, na nimekuwa nikichelewa. Kwa juu habari hiyo inaonkana kuwa kituko. Umewahi kuamini kitu chochote ambacho kamwe hakikuleta mantiki? Kitu ambacho hakina chembe ya ushahidi? Haya tunayaita kuwa ushirikina. Biblia inasema nini juu ya imani? Je, ni zaidi ya ushahidi? Je, tutarajie kusubiria maelfu ya miaka bila kuwa na uthibitisho vyovyote iwavyo kwamba sisi siyo wapumbavu? Au, imani ina mzizi wa kishuhuda ambao twaweza kuujenga hapo? Hebu tuingie kwenye Biblia ili tuweze kubaini!

I. Hakuna Ushahidi?
A. Soma Waebrania 11:1. Fungu hili linasema kuwa ni nini ambacho ni msingi wa kiushahidi wa imani yetu? (Matumaini yetu na vitu tusivyoviona.)
1. Mimi siyo mtaalam wa Kiyunani, lakini Waebrania 11:1 kwa Kiyunani yaelekea kusema juu ya imani kuwa ni “ushahidi usioonekana”. Je, hiyo yamaanisha kuwa watu ambao husema kuwa imani siyo ushawishi wenye vielelezo wako sahihi?
a. Au, ina maana kuwa kwa hakika kuna ushahidi wa imani, ni vile tu sisi siyo “mashahidi” kwa imani hiyo?

B. Soma Waebrania 11:3. Je, tu mashahidi katika hili? (Hapana).
1. Je, kuna kitu ambacho chaweza kuonekana hapa? (Ndiyo. Tunaona ulimwengu.)
2. Je, ni kweli kuwa ushahidi haupo katika imani yetu ya kwamba Mungu alifanya ulimwengu kwa amri yake? (Hatukuona Mungu akitenda hilo. “Amri” iliyotamkwa kwa maneno isingeweza kuonekana hata kama tungekuwa tunaangalia tendo hilo.)

C. Soma Zaburi 19:1-3. Je, Daudi na mwandishi wa Waebrania wana mtizamo tofauti?
1. Waebrania 11:3 inatuambia ya kwamba ni kwa imani pekee tunaamini kuwa Mungu aliumba ulimwengu. Mfalme Daudi anasema kuwa mbingu zinatoa kauli za uthibitisho (“zauhubiri,” “laitangaza”) juu ya Mungu wetu Muumbaji. Kila mmoja husikia na anaweza kuelewa ujumbe huu. Upi kati ya ujumbe wa Daudi na wa Waebrania una hoja nzuri zaidi?

D. Angalia mazingira yanayokuzunguka. Ushahidi unaouona kila siku unakuambia nini juu ya kama ulimwengu uliibuka au kama ulikuwa na Mbunifu Mahiri?
1. Je, ni kwa jinsi gani bustani yako inastawi bila juhudi za kibinadamu?
2. Je, ni kwa jinsi gani nyumba yako inastawi bila juhudi za kibinadamu?
3. Je, gari lako linadumu vipi bila juhudi za kibinadamu?
4. Je, kazi yako inafanikiwa vipi bila juhudi za kibinadamu? (Sijui kuhusu wewe, lakini eneo langu, nyumba yangu, gari langu na kazi yangu mara zote huhitaji uangalizi wangu-hii ni kusema kuwa haziwezi kuendelea bila “uwezo wa akili ya nje”. Kama hakuna mwanadamu ambaye angeingilia kati, vingekoma bila kutoa matokeo.

E. Mtizamo wangu ni kwamba maelezo ya kisayansi yanayoendelea sasa kuhusu ulimwengu ni The Big Bang Theory ambapo ulimwengu ulilipuka kutoka sehemu moja katika tukio moja la mlipuko. Ni nini ushahidi wa kisayansi katika hili? (Ulimwengu unatanuka sawia katika pande zake zote).
1. Je, huu pia ni ushahidi kuwa Mungu Muumbaji wakati fulani alizungumza na ulimwengu ukatokea?
2. Wanasayansi wanaamini kuwa kiwango cha utanukaji wa ulimwengu ni wa msingi Kama ungetanuka kwa haraka sana nguvu za uvutano zingefifia na ulimwengu unge “lipuka”. Na kama ungetanuka kwa pole pole sana, nguvu za uvutano zingezidi za utanukaji na ulimwengu ungesinyaa. Je, huu ni usahidi wa tukio la bahati “bang” au ushahidi wa Mbunifu ambaye kwa hakika aliweka kiwango cha utanukaji?

F. Soma Waebrania 11:4. Je, Habili hakuwa na ushahidi wa imani yake kwa Mungu? (Alikuwa na ushahidi wote uliomzunguka. Kielelezo ni kwamba Mungu aliongea moja kwa moja na Kaini na Habili (Mwanzo 4:6)).

1. Kwa hiyo, ni nini kwa hakika kilikuwa kiini cha imani ya Habili? (Imani yake ilikuwa kwa Mungu. Imani kwa Mungu ndio kilikuwa kiini cha imani ya Habili.)
2. Tunaambiwa ya kwamba Habili angali akinena. Anasema nini kwako? Kutokana na hicho anachokisema, unajenga imani yako juu ya nini? (Kisa kifupi cha Habili (Mwanzo 4:1-10) kina kila aina ya kauli kuhusu imani. Kinatuambia ya kwamba kumkataa Mungu hutuelekeza kwenye dhambi mbaya zaidi. Pia kinatuambia kwamba kumtii Mungu yaweza isimaanishe kuwa tutakuwa na maisha manyoofu. Kinapendekeza kuwa Mungu atatushindia kadri muda uendavyo).

II. Mfano wa Kwanza wa Imani: Tomaso

A. Soma Yohana 20:19-25. Je, Tomaso alikuwa na ushahidi wowote kwamba Yesu alikuwa amefufuka? (Ndiyo. Alikuwa na ushuhuda wa kuaminika wa watu kadhaa walioshuhudia).
1. Ni aina gani ya ushahidi ambao Tomaso alikuwa akiudai (Ushahidi wa kushuhudia binafsi).

B. Soma Yohana 20:26-29. Ni aina gani ya imani ambayo Yesu anaipendekeza? (wale ambao hawajaona lakini wakaamini).

1. Je, Yesu anahitaji imani isiyokuwa na tafakari wala mantiki? (Vitu viwili. Kwanza, Yesu anampatia Tomaso kwa hakika aina ya uthibitisho alioutaka. Pili, watu “waliobarikiwa” ni wale wanaoamini kwa misingi ya ushuhuda wa wengine. Yesu hahitaji wafuasi wake kuhisi kwamba alifufuka.

III. Mfano wa Pili wa Imani: Wewe

A. Soma 1 Petro 1:3-5. Fungu la 5 linatuelekeza kwetu sisi kukingwa ngao ya “imani”. Tunakingwa dhidi ya nini? (Soma 1 Petro 1:6. Imani yetu inatukinga na ukatishwaji tamaa pale ambapo maswahibu mazito yanapotokea).

1. Angalia tena 1 Petro 1:3-5. Msingi wa imani yetu ni nini? (Ya kwamba Mungu atatupatia maisha mapya katika nchi mpya. Tumaini letu katika hili limejengwa kwenye ufufuo wa Yesu kutoka katika wafu).

B. Soma 1 Petro 1:8. Je, tu mashuhuda wa ufufuo wa Yesu? (Hapana).

C. Soma 1 Petro 1:10-12. Je, hatuna ushahidi wa ufufuo wa Yesu? (Hapana. Tuna kauli ya Petro juu ya hili. Lakini, zaidi ya hilo, tuna unabii uliotimia kumhusu Yesu. Manabii wa Agano la Kale waliongea nasi pale walipoandika unabii kumhusu Yesu).

IV. Mfano wa Tatu wa Imani: Yairo

A. Soma Luka 8:40-42.je, Yairo alikuwa na imani? Imani yake ilikuwa juu ya nini? (Imani yake (tumaini?) ilikuwa ni kwamba Yesu angemponya bintiye mgonjwa).
1. Je, imani ya Yairo haikuwa na mantiki?

B. Soma Luka 8:43-49. Je, Yairo ana ushuhuda kwamba Yesu atamsaidia? (Alikuwa na ushahidi, lakini sasa ushahidi wote ni bayana na kwamba Yesu amemwangusha).

C. Soma Luka 8:50. Je, Yairo ana imani sasa kuwa Yesu atamsaidia?
1. Kama umesena ndiyo, ushahidi huo ni nini?

D. Soma Luka 8:51-56. Hali ya imani ya waombolezaji ilikuwaje kabla ya fungu la 54?
1. Angalia fungu la 56. Ni nini kiwango cha imani ya Yairo? (Wazazi wake wakastaajabu-ambayo inaashiria kuwa Yairo hakuwa na imani ya kwamba binti yake angefufuliwa kutoka katika wafu).

E. Je, kisa hiki cha mwisho kinatufundishaa nini kuhusu imani yetu kwa Mungu na hali ya ushahidi wa imani yetu? (Kwanza, inatuonyesha kwamba hata kama ushahidi unaonyesha kuwa Mungu ametuangusha, imani yetu sharti isubirie wakati/muda muafaka wa Mungu. Pili, Yairo alikuwa na ushahidi katika nguvu za Yesu-endapo ni kwa sababu ya uponyaji wa yule mwanamke aliyemchelewesha Yesu hadi kusababisha binti yake akafariki. Kilichotakiwa kwa imani isiyoonekana kilikuwa ni kiwango cha muujiza-ufufuo!)

F. Rafiki, kuna ushahidi mwingi wa imani. Je, waweza shikilia imani yako, hata kama hauna ushahidi ulioshuhudiwa kwa macho, au kile ukionacho ni ushahidi tofauti? Kama ukisubiria, kwa imani, Yesu atakupa uzima wa milele kama ukijihisi unaanza kutia shaka tazama ulimwengu na uumbaji na ujiulize kama vitu hivi vingeweza kuwepo kwa bahati.

V. Wiki Ijayo: Tumaini

Imefasiriwa na kutumwa na Mgune Masatu.