Friday, June 5, 2009

Lesoni somo la 11: Uwakili


(Mathayo 25)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sememu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani, Kihispania, Kizulu, nk.


 

Utangulizi: Mpangilio wa masomo haya unakwenda kinyumenyume, sawa? Tulifurahia somo kuhusu siku ya kupumzika katika kila wiki, baadaye tukajifunza kuhusu likizo ya milele, mbinguni. Wiki iliyopita tulianza kufanyia kazi "uanafunzi," na sasa (vitisho) "uwakili!" Je,isingefaa kuishia na mada zenye kusisimua zaidi? Au, je, uwakili ni mada inayosisimua? Popote pale maafisa wanapokuja kanisani kwangu kujadili uwakili, mara nyingi huwa inamaanisha kuwa wanataka pesa zaidi au kufanya kszi zaidi kutoka kwangu. Lakini, nadhani tutagundua juma hili kuwa Biblia ina njia chanya zaidi katika wazo hili. Hebu tujitose katika Biblia yetu na kujifunza kuwa ni nini uzuri kuhusu uwakili!

  1. Ushindi Maishani
    1. Soma Mathayo 25:14-15. Ni katika msingi upi bwana alitoa pesa nyingi kwa mtumwa mmoja zaidi ya mwingine? Je, ilikuwa ni upendeleo tu? (Hapana. Kiasili, watumwa walitofautiana katika uwezo wao. Alimpatia mtumwa mwenye uwezo mkubwa kwa asili pesa nyingi.)
      1. Je, hiyo haikuwa haki? Si kwamba kila mmoja apate kiwango sawa cha pesa?
        1. Au, je, haikuwa haki kwa mtumwa mwenye uwezo mkubwa wa talanta kwa asili kwa sababu sasa alikuwa na changamoto kubwa?
    2. Soma Mathayo 25:16-18. Je, kuna mjadala wowote kwa njia ya yule kijana wa "talanta moja"? Je, ni nini kuhusu anguko la hivi karibuni la soko la hisa? Ni nini kuhusu wasiwasi wetu katika taasisi zetu za kibenki? Je, tundu katika ardhi haliwezi kuwa mahali salama zaidi pa kutunzia mtaji?
      1. Je, kuna sababu yoyote ya kuamini kwamba yule mtu mwenye talanta moja alikuwa haenendi katika imani njema? (Ndiyo. Kama bwana alitaka pesa yake ihifadhiwe kwa kuificha, angeificha yeye mwenyewe-na asingehatarisha kuruhusu yule kijana mwenye talanta moja kujua pale ilipo.)
    3. Soma Mathayo 25:19-23. Kwa nini yule kijana aliyetoa talanta mbili zaidi anapata sifa sawa na kijana yule aliyetoa talanta tano zaidi? Je, hiyo ni haki? (Wote wawili walileta talanta mara mbili zaidi katika zile walizopewa. Hii inamaanisha kwamba, kwa kuwa bwana aligawa pesa kwa kuangalia katika uwezo wao wa asili, bwana hatoi adhabu kwa upungufu wa talanta ya asili. Suala siyo kuwa ni talanta gani unazokuwa nazo wakati unapozaliwa, suala ni unafanyia nini hizo talanta zako.)
    4. Soma Mathayo 25:24. Hii inafunua hali ya kiakili ya yule kijana mwenye talanta moja. Kwa nini anamuita bwana wake majina ("mtu mgumu")?
      1. Je, si kweli kwamba mtu mmoja asipate faida kutokana na bidii ya kazi ya mtu mwingine? Je, huu siyo "unyonyaji?"
    5. Soma Mathayo 25:25. Hebu subiri, je, yule mtu mwenye talanta moja amebadili kisa chake? (Ndiyo. Sasa anadai kwamba alikuwa anaogopa. Kwanza, anadai kuwa bwana wake ni bepari, halafu anadai kuwa anaogopa.)
    6. Soma Mathayo 25:26-27. Je, bwana anachanganua vipi suala hili? Je, yule kijana mwenye talanta moja ni mwoga? Je, ana malalamiko halali kuhusu mabepari? (Bwana anamuita "mbaya na mlegevu.")
      1. Je, bwana yupo sahihi kwa kijana huyo kuwa "mbaya?" Nilifikiri kuwa yule kijana mwenye talanta moja alikuwa anadai pingamizi la kimaadili. (kama ambavyo inadhaniwa kuwa ubepari ni uovu mbele za Mungu! Neno "ubaya" bila shaka lina maana kuwa mtumwa na wajibu wa kuendeleza hatma ya bwana. "Ulegevu" unahusika kwa sababu hakufanya jambo lolote.)
    7. Soma Mathayo 25:28-30. Kwa nini yule kijana mwenye talanta kumi apate fedha kidogo alizokuwa nazo yule mwenye talanta moja? Sasa yule kijana mwenye talanta kumi "amejawa" wakati yule mwenye talanta moja hana kitu. Je, hii ni haki? (Tutachanganua siri hiyo katika sehemu inayofuata pale tutakaposoma Mathayo 25:34-40.)
    8. Hebu turudi nyuma kidogo na kuangalia kisa hiki. Yesu anatufundisha nini? Je, ni kuhusu fedha, talanta, na wakati/muda? Hili ni "fumbo la kimbingu." Visa vyote hivi katika sura hii vina jambo la kufanya kuhusiana na njia za kwenda mbinguni.)
      1. Pale ambapo inatokea "kijana wa uwakili" anajitokeza, hisia zangu ni kwamba ataishia kuwa na vingi nami nitaishia kuwa na vichache. Kisa hiki chatufundisha nini kuhusu uwakili? (Kisa kinarejea hususan fedha, lakini nafikiri kinawakilisha/kinamaanisha aina zote za talanta za asili. Njia ya kuelekea kwenye "wingi" ni kuweka talanta na fedha zako katika kazi (Mathayo 25:16). Kitu kikubwa ni kwamba haijalishi kuwa ni talanta ngapi unapewa mwanzoni. Kinachojalisha ni kile unachozifanyia. Kama u mwaminifu, utajaaliwa na nyingi. Uwakili ni kuhusu kuwa na vingi.)
  2. Kuwajali Masikini
    1. Soma Mathayo 25:31-40. Je, kijana mwenye talanta moja, hususan baada ya kuwa ametupwa nje na bwana bila fedha zake, astahili kama (fungu la 40) "wa hao ndugu zangu walio wadogo?"
      1. Hebu jifanye kwamba wewe ni (kwa sasa) kijana mwenye talanta kumi na moja (bwana amekupatia hivi punde tu ile talanta ya kijana mlegevu na mbaya), na unakumbana/unagongana (sasa) na kijana asiye na talanta. Je, Yesu anafundisha kwamba umpatie pesa huyu kijana asiye na talanta?
        1. Je, hiyo haitafanya bwana afanye uamuzi kwa kura ya turufu?   
        2. Unadhani inaleta tofauti yoyote kwamba kisa hakitaji fedha? Mwenye njaa anapata chakula, mwenye kiu maji, mgeni anapata ukaribisho, wale wanaohitaji nguo mpya wanapata nguo. Kwa nini hakuna yeyote anayepata fedha? (Kisa cha talanta kilichotangulia kwa hakika kinaonyesha fedha. Kisa hiki kamwe hakionyeshi fedha. Kama tuko sahihi kwamba kumpatia kijana "asiye na talanta" wa sasa fedha baada ya bwana kuwa ameichukua inaweza kuwa tatizo, basi kugawa mahitaji ya kijana asiyekuwa na talanta hakutaleta maana.)


 

  1. Je, inawezekana kwamba hata kama Yesu anarejea/ananukuu fedha katika fumbo la kwanza, ni ya kiishara na inahusika na fedha kwa uchache/udogo? (Kama ukiangalia Mathayo 13:12, utakuta kauli ile ile "kuwaongezea wenye juhudi, kuwanyang'anya walegevu" ikiwa katika muktadha wa kiroho.)
  2. Je, inawezekana kwamba pale ambapo mtu mwenye talanta kumi na moja anapomsaidia kijana asiyekuwa na talanta kwamba bado anawekeza talanta zake? (Hatuambiwi jinsi talanta zilivyowekezwa. Kama hili linatumika kiroho, basi inaleta maana kwamba talanta zinawekezwa katika masuala ya kimbingu).
  1. Nimeuliza maswali kadhaa kukufanya utafakari kuhusu kile Yesu anachotufundisha. Ni masomo gani ambayo tunaweza kuwa na uhakika nayo katika haya mafumbo (hii mifano) mawili? (Kwamba Mungu anatutaka kuwa wenye bidii katika kumtumikia. Kwamba sehemu ya kazi yetu ni kuwasaiia wale walio wahitaji.)
  1. Asili ya Talanta
    1. Tumegundua kwamba Yesu alielezea mafumbo (mifano) yaliyolinganisha talanta zetu (ambazo kwazo lazima tuwe na bidii nazo) katika fedha na bidhaa nyinginezo. Je, talanta zetu pia zinajumuisha uwezo wetu wa asili? (Angalia tena MAthayo 25:15. "Kila mtu kwa kadri ya uwezo wake" lazima irejee uwezo wa asili. Uwezo wa asili ulikuwa ndio ufunguo wa kiasi cha fedha kilichotolewa na bwana.)
    2. Soma Mathayo 24:45-51. Hiki ni kisa kingine cha bwana aliyesafiri. Ni rasilimali gani ambayo mtumwa anatakiwa kuitolea hesabu hapa? (Uwajibikaji na wakati/muda. Kwa sababu "bwana anakawia" mtumwa anaamini kuwa ana muda wa kuwanyanyasa wale walio chini yake na kupoteza muda wake mwenyewe.)
      1. Je, muda ni talanta ambayo tunapaswa kuwa mawakili wazuri? (Ndiyo. Hata hivyo, ukweli kwamba Mungu aliumba hitaji la wanadamu kulala inaonyesha kwamba usawa fulani kati ya kazi/uwajibikaji na pumziko unahitajika.)
        1. Ni asilimia ngapi ya muda wako unatumika katika kuendeleza masuala yako mwenyewe tofauti na masuala ya wengine?
        2. Ni asilimia ngapi ya muda wako unapotea na hautumiki kumsaidia mtu yeyote?
        3. Je, kuwanyanyasa na kuwapotezea muda watu wengine linaonekanaje kwa huyu mtumwa? (Siyo mzuri. Mwisho mwingine wa "kulia na kusaga meno".)
    3. Rafiki, tunaona kwamba wafuasi wa Yesu wenye juhudi wanafanikiwa na wafuasi walegevu na watapanyaji hulia na kusaga meno yao. Ninatafsiri "kusaga meno" kama majuto kwa maamuzi yaliyofanyika kipindi cha nyuma. Una maamuzi ya kufanya kwa ajili ya siku zijazo, je, utaamua kuwa mtumwa mwaminifu na mwenye juhudi wa Yesu?
  2. Wiki Ijayo: Jumuiya.


 

Imetafsiriwa na kuandaliwa na

Mgune Masatu.

No comments:

Post a Comment