Wednesday, April 22, 2009

Lesoni Somo la 4: Uzima

(Yohana 10, Matendo 27 & 28, Luka 12)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani, Kihispania, Kizulu, nk.

Utangulizi: Je, umewahi kutafakari juu ya maisha yako? Yana mwelekeo gani? Ungependa yawe na mwelekeo gani? Pamoja na kazi zetu, luninga, mtandao, watoto, kazi za nyumbani, na utume/ujumbe, ni rahisi kujishughulisha na “masuala ya haraka” kwa muda wa siku nzima. Tupatapo muda wa kupumzika, tunautumia kwenye kitu kingine zaidi ya kukaa na kutafakari tu. Huenda tafakari ni kitu kinachofananishwa na yoga tu, kwa jinsi tunavyojihusisha, na si sehemu ya maisha yetu. Hebu tuchukue wasaa na kutafakari, kupitia kwenye maaandiko ya Biblia, kile inachomaanisha kuishi. Hebu na tuangalie malengo aliyonayo Mungu kwa ajili yako!


I. Kipofu na Anayeona

A. Katika Yohana 9, Yesu anamponya kipofu. Hiyo iliamsha mtafaruku kwa viongozi wa dini. Hebu tuangalie kisa hicho mwishoni mwa Yohana 9. Soma Yohana 9:39-41. Yesu anasema kuwa amekuja ulimwenguni humu kwa hukumu. Je, Yesu alikuja ulimwenguni kutuhukumu? (Soma Yohana 3:17-18. Yesu alikuja kuuokoa ulimwengu).

1. Kama Yesu hakuja kuuhukumu ulimwengu, je, ni aina gani ya hukumu ambayo Yesu anaiongelea katika Yohana 9:39? (Tunajua ya kwamba Yesu alikuja kufa kwa ajili ya dhambi zetu. Kwa hiyo, hukumu ni lazima, angalao kwa kiwango fulani iwe juu yake).

2. Ni aina gani ya hukumu itakayofanya vipofu waone na wale wanaoona kuwa vipofu? (Mungu aliye na nia ya kutuponya, Mungu aliye na nia ya kufa kwa ajili yetu, Mungu ambaye anaonyesha huruma kwetu hufungua macho yetu kuhusu asili ya Mungu. Mwovu ambaye analeta upofu, na anayejeruhi na kuua, Mungu hufungua macho yetu kuhusu asili ya pambano kati ya wema na uovu).

3. Ikiwa sasa tumeshamwona Yesu, je, tunahitajika kufanya nini? (Yesu anafundisha kwamba mara tunapoelewa masuala ya kiroho, basi tuna uamuzi wa kufanya ili kuzuia hatia- na hukumu).

B. Soma Yohana 10:1-2. Kama ningekuwa natizama kwenye nyumba ya jirani yangu, na nikaona mtu fulani akiingia kwenye nyumba hiyo kupitia dirisha lililo nyuma ya nyumba, je, nifikirie juu ya kitu gani? (Huyu ni mtu asiye na ufunguo. Huyu ni mtu asiye na mamlaka husika).

1. Ni nini malengo ya nyumba yenye mlango na kitasa? Lengo la zizi la kondoo na lango ni nini? (Ni kulinda viumbe vinavyoishi humo, kuhifadhi watu wanaohusika ndani na wasiohusika nje).

1. Je, hili lina uhusiano gani na mazungumzo ya Yesu juu ya upofu? (Yesu anasema kuwa Mafarisayo ni vipofu-au angalao basi wanatenda/wanajifanya kuwa wao ni vipofu. Yesu anatuambia kuwa kuna ukweli ulio dhahiri katika maisha-kama vile ukweli kuhusu milango-kwa wale walio na nia ya kutizama).

A. Soma Yohana 10:3-6. Je, u mbele ya wanafunzi wa Yesu kimtizamo hapa? Naelewa kile ambacho Yesu anasema kuhusu zizi la kondoo-ambacho tunaweza kulinganisha na majumbani mwetu-lakini je, tunalitumia vipi hili katika maisha yetu? (Hebu tuendelee kusoma).

B. Soma Yohana 10:7. Sasa tunaelekea pahala fulani. Kama Yesu ndiye lango, je, zizi ni nini na kondoo ni akina nani? (Nadhani sisi ndio kondoo. Zizi lazima liwe ulinzi wa maisha yetu. Yesu huruhusu watu sahihi kuingia zizini na kuwaweka wasiostahili nje ya zizi.

C. Soma Yohana 10:8-9. Wawezaje kulitumia hili maishani? (Kama Yesu ndiye lango la kuingilia lililoidhinishwa, na malango mengine yote ya kuingilia yanatumiwa na watu wenye kuleta madhara, hii humaanisha kwamba Yesu ana njia za kulinda na kuwezesha/kufanikisha maisha yetu. Ni kama nyumba salama iliyo na lango la kuingilia linaloangaliwa/lindwa.

D. Soma Yohana 10:10. Kama ningesema kuwa ningeweza kukupatia “maisha kamili,” ungeelewa kuwa hiyo inamaanisha nini?

1. Yesu amekuwa akiongea nasi kuhusu njia na ulinzi, je, maisha kamili yanahusianaje na hilo? (Kama unaishi maisha sawasawa na mafundisho ya Mungu (Yeye ndiye lango pekee kwa kile unachokiruhusu kupita kupitia kwenye lango hilo) una maisha yaliyo makamilifu).

a. Je, hii ni kweli? Kuna kila aina ya programu za kwenye luninga zinazonifundisha kwamba maisha makamilifu na yenye furaha yanahusisha vitu vingine zaidi ya vile vilivyvothibitishwa na Mungu. Je, kuna ukweli mwingine?

b. Ni nini juu ya watu ambao wanaamua kwamba wataishi kama vile wanavyotaka sasa na watamrudia Mungu baadaye? Je, kuna ukweli wowote juu ya hilo?

E. Soma Yohana 10:11-13. Kwa nini mtu anayelipwa/aliyeajiriwa hafanyi kazi nzuri? Je, sisi sote si “waajiriwa” pale inapokuja kwenye kazi zetu? (Walioajiriwa huangalia vitu kimantiki-kupoteza maisha yake hakuwezi linganishwa na mshahara wake. Kama akiyatoa maisha yake, atakuwa na kitu gani hapo sasa?).

1. Ni nini hoja ya Yesu kwa ajili ya maisha yetu? (Yesu hafanyi hili kwa ajili ya kupata pesa. Alionyesha kwamba alitujali kwa kuyatoa maisha yake kwa ajili yetu).

2. Hili lina nini cha kufanya nasi kuwa na wakati mzuri sasa kwa kutenda yale mambo ya kufurahisha tunayoyaona kwenye luninga? (Mambo “yote mazuri” yaonekanayo kwenye luninga huhusisha uajiriwa. Njia ya ulimwengu ni kuamua kile kilicho bora kwa “namba moja.” Misukumo inapokuja, wengine huishia kuumia/kupata mateso/mahangaiko.

3. Ni nini hoja ya msingi ya kiroho inayoweza kuonekana hapa? (Kama tutatizama, na kutokuwa vipofu, tutaona ya kwamba maelekezo ya Mungu kwa ajili ya maisha yetu yanabubujika kutoka kwenye upendo ulio mkubwa kiasi kwamba yu tayari kuyatoa maisha yake kwa ajili yetu. Hakuna hata mtu mmoja anayetoa “ukweli” unaodhihirishwa na programu ya luninga iliyo maarufu inajali kile kitakachotutokea. Wanajalisha juu ya kupata fedha kutokana na program hizo. Haijalishi ni masomo gani tunayojifunza kutokana na program hizo, hiyo siyo wajibu wao-walao hivyo ndivyo wanavyoliangalia suala hilo.

F. Soma Yohana 10:14-18. Je, Yesu analazimishwa kufa kwa ajili yetu? (Hapana! Tazama hoja ambayo Yesu anaifanya. Aliyatoa maisha yake kwa ajili yako. Kwa nini angekupa maelekezo ambayo yanaweza kukuangamiza? Maelekezo ambayo yangeweza kuwa na ukomo wa kuishi maisha makamilifu? Asingeweza. Lakini, mbwa mwitu na waajiriwa hawakujali. Sheria zao za kimaisha haziakisi hilo.

G. Kama ungeweza kutafakari kwa kitambo kifupi juu ya maisha yako na jinsi ambavyo ungeishi, je, uamuzi wako wa kichoyo ungekuwa upi? (Uamuzi wa kumfuata yule aliyekuwa na nia ya kufa kwa ajili yako! Kama ungetaka kufanya kile kilichokuwa bora kwa ajili yako, basi ungekataa ushauri wa wale ambao maslahi yao ni kwa ajili yao-siyo kwako.

1. Je, hitimisho hili lina ukomo kwa masuala ya kiroho? (Hapana! Yesu alitumia mpango-kutunza kondoo-kama mfano wake. Ushauri huu unahusika katika nyanja zote za maisha kama tutakavyoona katika sehemu inayofuata).


II. Maisha Yenye Ushawishi wa Kweli

A. Utakumbuka ya kwamba wakati Paulo alipokuwa akihubiri injili, alifungwa na alikata rufaa Roma. Akiwa kama mfungwa, aliwekwa kwenye mashua pamoja na kundi la wafungwa wengine wakielekea Roma.

B. Soma Matendo 27:10-12. “Nyanja zipi za ushawishi” zinahusishwa katika kisa hiki? (Tunaye Paulo anayemwakilisha Mungu na maslahi ya kiroho. Tunao wamiliki wa mashua wanaowakilisha maslahi ya kibiashara. Tunaye jemadari anayeiwakilisha Serikali.

1. Kama ungekuwa Paulo, na ungetaka maisha yako yawe na ushawishi kwenye biashara na Serikali ungedhani juu ya kitu gani kama kikwazo cha mafanikio katika wasaa huu? (Yeye ni mfungwa!).

a. Je, ushauri wa Paulo umezingatiwa? (Hapana).

C. Soma Matendo 27:14-20. Ni nini ambacho hakikufanya kazi kuhifadhi maslahi ya biashara na ya Serikali? (Nyenzo zao wenyewe).

D. Soma Matendo 27:21-26. Mungu anatendaje kazi kupitia kwa Paulo kushawishi biashara na Serikali? Je, ni kitu gani ambacho Paulo hakukifanya? (Paulo hakusema kuwa “Mungu ameleta hukumu kwenu”. Badala yake malaika alimjia Paulo na kumpa suluhisho la tatizo. Paulo alikumbushia biashara na Serikali ambapo hapo awali alikuwa amewapa ushauri sahihi).

1. Kama unataka kushawishi juu ya biashara na Serikali, je, unahitaji kuwa na silaha za aina gani? (Malaika za Mungu! Roho Mtakatifu. Udhibiti wa Mungu wa Matukio).

E. Soma Matendo 27: 30-32. Ni nani sasa anayeshikilia juu ya operesheni ya biashara na Serikali? (Mtu wa Mungu, Paulo).

1. Ilichukua muda gani kubadilisha hali ya kutofuata ushauri wa Paulo na kumfuata Paulo?

F. Soma Matendo 28: 1-4. Ni siku ya aina gani aliyonayo Paulo hapa? Ulimwengu unamwona Paulo kuwa ni mtu wa aina gani?

G. Soma Matendo 28:5-6. Ni nini mtazamo wa ulimwengu dhidi ya Paulo sasa? Ilichukua muda gani kufanya badiliko hili?

H. Soma Matendo 28:7-9. Paulo sasa anakumbana na Serikali ya Malta. Ni aina gani ya ushawishi ambao Paulo anaupa msukumo kwenye uongozi wa Serikali?

I. Ni somo gani ambalo kisa hiki kinatufundisha kuhusu kufuata sheria za Yesu tunapojihusianisha na biashara pamoja na Serikali?


III. Kutokuwa na Woga/Wasiwasi

A. Soma Luka 12:22-26. Angalia hususani fungu la 25. Jibu lake ni nini?

1. Ni vipi kama ningeuliza swali hilo tofauti: ni nani, kwa kudhibiti (mlo, uvutaji sigara, mazoezi, kuendesha gari, hasira) yake, anaweza kuongeza saa moja katika maisha yake? Ni wangapi kati yenu mngejibu “ndiyo” kwenye swali hilo?

a. Ni nini sasa, ulio muktadha wa kuishi maisha yasiyokuwa na wasiwasi? (Sidhani ya kwamba Yesu anatuambia twende tukalale chini ya madawati. Wakolosai 3:23-24 inapendekeza kinyume chake. Ufunguo wa maisha kamili na yasiyokuwa na wasiwasi unatokana na kufuata sheria za Mungu na kuacha mengine yote kwa Mungu).

B. Rafiki, chukulia jinsi ambavyo maisha yangekuwa kama ungeamua kuwa njia ya Mungu ndio mara zote ingekuwa ya kufurahisha kuliko kitu chochote, ya kupendeza zaidi ya chochote? Chukulia jinsi ambavyo maisha yako yangeweza kuwa na ushawishi wa juu kabisa kwenye biashara na Serikali. Kumtumikia Mungu kwa moyo wako wote ndio njia kuelekea kwenye maisha yasiyokuwa na woga/wasiwasi, maisha yenye mafanikio na ushawishi mkubwa! Je, utachagua njia ya Mungu leo?


IV. Wiki Ijayo: Ufunuo.

No comments:

Post a Comment