Friday, July 10, 2009

Lesoni ya 3: Kutembea Nuruni: Kugeuka na Kuacha Dhambi



(1 Yohana 1)


Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sememu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani, Kihispania, Kizulu, nk.

Utangulizi: "Ina tatizo gani?" Umeshawahi kujiuliza hilo swali pale ulipotaka kufanya jambo lenye mashaka (linaloweza kujadiliwa)? Je, watoto wako wamekuuliza hilo swali pale walipotaka kufanya jambo ulilowazuia? Biblia inafundisha kwamba kuna wigo mpana wa maamuzi ambao hauhusishi dhambi. Wakristo wanaweza kutokubaliana kwa kutumia akili (kwa kutafakari kwa makini) kama baadhi ya matendo ni dhambi, na kila upande unaweza kuwa sawa. (Angalia Warumi 14.) Wakati huo huo, Yohana anatufundisha kuhusu umuhimu wa maamuzi yetu yote. Analinganisha maisha na kufanya matembezi. Je, kila maamuzi maishani yanatupeleka karibu zaidi na haki au karibu zaidi na dhambi? Hebu tujivinjari katika somo letu na kubaini! Tunaweza kuamua kama "Ina tatizo gani?" ni swali sahihi au la.

  1. Nuru = Mungu
    1. Soma 1 Yohana 1:5. Wiki iliyopita tulijadili kwa nini Yesu anaelezewa kama "Neno la Uzima." Sasa katika 1 Yohana 1:5 tuna neno jipya kumhusu Yesu, "Nuru." Unafikiri kwa nini Mungu anaelezewa kama "Nuru?" Kwa nini neno hili lahusika au ni maelezo sahihi kumhusu Mungu?
      1. Nini kinakujia mawazoni pale unapofikiri kuhusu nuru? (Nguvu/uwezo. Uwezo wa kuona. Jukumu. Uwazi.)
      2. Yesu anasema "Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe." Yohana 8:12. Hii inapendekeza nini kuhusu asili ya "nuru" ya Mungu? (Ya kwamba inatusaidia kuelewa ukweli kutokana na uongo [wema kutoka kwenye uovu]).
    2. Wiki iliyopita tulijadili kwamba sababu moja kwa nini "Neno" yalikuwa ndio maelezo sahihi kumhusu Yesu ni kwamba aliumba ulimwengu kwa kutamka tu, kwa "neno". Tukitafakari kwenye uumbaji tena, nini kiliumbwa kwanza? (Mungu alitamka "nuru" nayo ikawa. Mwanzo 1:3). 
      1. Unaona uhusiano kati ya tendo la kwanza la Yesu la uumbaji na kile anachoitwa? (Nuru humwelezea Mungu. Alituumba kwa mfano wake. Kwa hiyo ni kawaida kwamba pale alipoanza "kutamka" uumbaji alianza na nuru.)
    3. Angalia tena 1 Yohana 1:5. Yohana anasema kwamba hamna giza lolote ndani ya Mungu. Kwa nini hili ni muhimu? Kwa nini kipengele hiki kiongezwe? (Sababu tatu: Kwanza , miungu iliyokuwepo wakati huo ilikuwa na upande muovu pia. Ilikupasa kuwa makini jinsi ulivyohusiana nayo kwa sababu ungeweza kuamsha hisia za hasira tena isiyo ya haki. Pili, tunahitaji kujua asili ya ushirika wetu na Yesu. Sasa tunashirikiana na "mtu fulani" ambaye ni nuru kabisa – mwema kabisa. Tatu, uovu hautoki kwa Mungu.)
  2. Uchaguzi
    1. Soma 1 Yohana 1:6-7. Tafakari ya kwamba unatembea kwenye msitu mdogo (sehemu yenye miti mingi) na unafika njia panda. Unatakiwa kuchagua njia ya kufuata. Katika haya mafungu mawili Yohana anafafanua njia panda katika maisha. Kwa mujibu wa Yohana, ni chaguzi gani mbili zilizopo? (Tunaweza kuchagua nuru au tunaweza kuchagua giza .)
      1. Kwa namna nyingine, Yohana anaelezeaje chaguzi hizi? (Mwishoni mwa fungu la 6 linarejea jambo "ukweli." Kwa hiyo, tuna uchaguzi wa "kweli" ama "uongo.")
      2. Ni maneno gani mengine ungeweza kuyatumia kuelezea chaguzi hizi? (Vipi tukitumia "wema/uovu," njema/mbaya," "haki/isiyokuwa haki?")
    2. Angalia tena 1 Yohana 1:5. Kwa mujibu wa Yohana, ni nani ambaye ni muasisi wa hili wazo la kuwa na chaguzi mbili za maisha barabarani? (Yohana anaweka kijisehemu kidogo katika fungu la 5 kuhusu chanzo cha ujumbe wake. Anasema, "Na hii ndiyo habari tuliyoisikia kwake, na kuihubiri kwenu." Huyu "Yeye" ni nani? Neno la Uzima – Yesu!)
    3. Kama Mungu anasema kuna chaguzi mbili maishani, na Mungu yu bayana katika njia yenye nuru," je, hilo kimantiki halimaanishi kuwa kila amuzi linaangukia aidha kwenye uchaguzi mzuri au uchaguzi mbaya?
  3. Kujaribisha "Njia" Yako.
    1. Hebu tupitie upya. Yohana alianza kitabu chake (1 Yohana 1:1-4) kwa kusema kwamba alitutaka tuwe na ushirika na Mungu. Baadaye akatuambia kwamba maisha ni kama ujia/njia kwenye msitu mdogo/sehemu yenye miti mingi: Una nafasi ya kwenda kushoto au kulia. Ni njia moja pekee inayotuelekeza kuwa na ushirika na Mungu. Soma tena 1 Yohana 1:6. twawezaje kujua kama tupo kwenye njia sahihi? (Yohana anapendekeza "Kujijaribu mwenyewe.")
      1. "Jaribu" hili ni nini? (Kutembea gizani. Kama ukitembea gizani, haupo katika njia sahihi na hutokuwa na ushirika na Mungu.)
        1. Hebu subiri kidogo. Kuniuliza kama ninatembea "gizani" siyo ya msaada sana . Yohana anasema nini kutusaidia kujua kile inachomaanisha kutembea gizani? (Yohana anafafanua kwamba baadhi wanadai kwa uongo kuwa wanatembea nuruni. Unajaribisha hili kwa kuangalia kama wanaishi kwa kuifuata kweli.)
    2. Soma 1 Yohana 1: 8 & 10. Ni jaribu gani hili linalojaribisha kama tupo kwenye njia sahihi? ( Kama tutadai kuwa hatuna dhambi, tutakuwa katika njia potufu.)
      1. Je, hili ni jaribu la matendo yetu, kama katika 1 Yohana 1:6? (Hapana. Hili ni jaribu la mtizamo wetu, mafikara yetu. Badala ya kutumia neno "kudai" hebu tutumie neno "kufikiri" ili kulifanya liwe la binafsi zaidi.)
        1. Unafikiri huna dhambi?
        2. Kama utashindwa jaribu hili, matokeo yake ni nini? (Hatusemi ukweli. Hili linatuweka katika njia potofu – katika njia ya giza .)
        3. Unafikiri hawa watu wanajua kuwa wapo kwenye njia ya giza ? Kama mtu anadai kutokuwa na dhambi, ungedhani kuwa wasingekuwa watu "wema". (Baini tena maneno ya 1 Yohana 1:8. "Tunajidanganya." Watu hawa kwa hakika wanajidanganya kuhusu haki yao.)
      2. Ni katika mazingira yapi mtu au watu wangefikiri au kusema kuwa hawakuwa na dhambi? (Mtu ambaye angedai ukamilifu. Niliwahi kusikia binti mmoja aliyedai kuwa yeye ni nabii wa kisasa na pia kudai kwamba aliishi miezi sita iliyotangulia pasipo kutenda dhambi. Wale wanaodai kwamba tunaweza kuufikia ukamilifu katika matendo yetu wanatakiwa kutafakari fungu hili kwa makini sana.)
      3. Je, kuna mazingira mengine tena ambapo mtu anaweza kufikiri kuwa hakuwa na dhambi? (Kinyume cha hali ya ukamilifu ni kudai kwamba dhambi si dhambi tena kwa wenye haki. Hili ni wazo tunaloweza kulifanya tutakavyo, kwa sababu dhambi haihusiki tena kwa Wakristo. Dhambi haijalishi tena kwa sababu kwa namna fulani imebadilishwa katika haki. Yohana anasema kwamba dhambi ni dhambi na tunatakiwa kukiri/kukubali hilo.)
    3. Angalia tena 1 Yohana 1:10. Je, Mungu amekuwa akituongelea? Yohana anamaanisha nini pale anaposema kwamba madai kuhusu hulka/asili nzuri ya mwanadamu "humfanya [Mungu] kuwa mwongo?" (Mungu ametufunulia dhahiri hali halisi ya mioyo yetu. Katika Mwanzo 8:21 anatuambia kwamba kila "mawazo ya moyo [wetu] ni mabaya tangu ujana ujana." Katika Yeremia 17:9 anasema "Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaje kuujua?")
    4. Soma tena 1 Yohana 1:8. Je, hatuna tatizo lingine? Wale walio katika njia sahihi, njia "nyepesi" wanawezaje kuwa wadhambi, wenye mienendo mibaya na kuwa waovu tangu ujana?
      1. Kama kwa Mungu hakuna giza kabisa, na tunatakiwa kuwa katika njia ya Mungu, twawezaje kuwa na dhambi ndani yetu?
      2. Unakumbuka swali langu pale mwanzoni kuhusu kama maamuzi yote maishani yalikuwa masuala "sahihi/makosa"? Twawezaje kuwa katika njia sahihi hali tukiendelea kuchagua dhambi? Je, hili siyo "jaribu" la kama tupo katika njia sahihi – kuishi kwa kufuata kweli (1 Yohana 1:6)?
  4. Asili ya Kutembea
    1. Kutatua hili tatizo la mwisho, hebu tuchukulie kwa makini neno "tembea." Ulinganisho wa Yohana ni kati ya kutembea nuruni na kutembea gizani. Unafikiri  inamaanisha nini "kutembea" nuruni au gizani? (Kutembea humaanisha kusogea. Vines hutufundisha kwamba wakati ambapo neno hili linamaanisha kutembea katika hali halisi katika sehemu nyingi kwenye Agano Jipya, kamwe haimaanishi kutembea katika hali halisi katika nyaraka za Yohana. Vincent's anaongezea kwamba Yohana anaongezea kuhusu "hali ya maisha iliyozoeleka ambayo ni ngumu kuiacha." Kutokana na hili ninaelewa Yohana husema kuwa "desturi yetu" ni kutenda uovu au wema.)
      1. Je, hili linatatua tatizo la kimantiki kuhusu jinsi ambavyo tunaweza kuwa katika njia nyepesi na bado tukiwa na dhambi katika maisha yetu? (Ndiyo. Dhambi ni kukengeuka/kupotoka kwa kuiacha njia, lakini lengo letu ni kuwa na mwelekeo wa jumla, desturi yetu maishani, kuishi kwa kuifuata kweli.)
      2. Hii inapendekeza nini kuhusu dhambi na kila maamuzi tunayoyafanya? (Maamuzi yanaweza yasihusishe dhambi, lakini yumkini inatuelekeza kuelekea au mbali na dhambi. Hili ndilo wazo la "kutembea." 
    2. Leo hii tatizo kubwa ni kuliita giza nuru. Tatizo hili ni kubwa kiasi gani katika muktadha wa mafundisho ya Yohana? (Hatuwezi kujua kuwa tupo katika njia potofu, hatuwezi kuenenda kuelekea kwenye barabara ya mabadiliko/matengenezo, isipokuwa tu tukikiri/kubali kuwa dhambi ni dhambi. Kama tutaiita dhambi kuwa haki, mara zote tutaendelea katika njia potofu hadi pale itakapotuua.)
  5. Njia Iliyofaulu
    1. Soma 1 Yohana 1:9. Wadhambi wanawezaje kuendelea katika njia nyepesi? Kama Mungu hana giza , sisi wanadamu tena tulio wadhambi twawezaje kufaulu kutembea katika njia nyepesi? (Mungu atasamehe dhambi zetu zilizoungamwa. Yesu anatufaulisha kwa ajili ya njia nyepesi!)
    2. Je, wale wanaotembea nuruni wana upeo wa uelewa wa dhambi zao? (Ndiyo. Hii inaelezea mjadala wa yesu kuhusu wale wanaodai (kimakosa) kwamba hawana dhambi. Mungu asifiwe kwamba kuna suluhisho! Tupo katika njia kuelekea kwenye ushirika hata kama tuna dhambi. Ukweli kwamba una dhambi maishani mwako hakukuondoi kuwepo kwenye njia "sahihi." Lakini, kumbuka kwamba kama unatembea gizani, haupo katika njia sahihi. Uelekeo wa maisha yako unahusika.)
    3. Je, hali ikoje kwako rafiki? Je, waziungama dhambi zako bila kusita? Au nawe unadai kutokuwa na dhambi? Upo katika njia kuelekea kuwa na ushirika na Mungu au katika njia kuelekea kwenye giza la milele?
  6. Wiki Ijayo: Kutembea Nuruni: Kutunza Amri Zake.

 

No comments:

Post a Comment