Wednesday, May 13, 2009

Lesoni somo la 7: Neema

Neema
(Isaya 53, Warumi 5-7)

Maisha ya Mkristo: Somo la 7

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sememu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani, Kihispania, Kizulu, nk.

 
 

Utangulizi: pale ambapo rafiki yangu wa Kiebrania alipokuwa akijadiliana nami kuhusu dini, alidai ya kwamba wakristo "wemeteka nyara" dini yake. Katika kumjibu, nilisema kuwa "tumekamilisha" dini yake. Katika kujenga hoja yenye kuleta mantiki, nikamuuliza kuwa huduma ya mahali patakatifu na kutolewa kafara kwa mwana-kondoo, yote hiyo ni juu ya nini? Kama ilikuwa tu ni juu ya kuchinja wanyama ili kutuondolea dhambi, je, ni kwa nini sasa tusiendelee na utamaduni huu? Sio lazima kuwa na kafara hekaluni! Hebu tafakari juu ya hili: Judaism (dini ya Kiyahudi), Uislam na Ukristo, zote hizi hukubali neno la Mungu kutoka katika Agano la Kale, lakini ni Ukristo peke yake unaokamilisha mantiki inayounganishwa na neema. Yesu, mwana-kondoo wa Mungu, anazichukua dhambi zetu. Hicho ndicho kile inachokizungumzia. Hebu tujivinjari kwenye somo letu la neema tuweze kujifunza zaidi!

  1. Neema Yatabiriwa
    1. Siku za hivi karibuni, nilikuwa na watu kadhaa waliokuwa wanapendekeza kwangu kuwa muungano kati ya Yesu na manabii wa Agano la Kale ni mdhaifu. Hebu tuchunguze hili kwa kusoma Isaya 53. Soma Isaya 53:1. Kuna tatizo gani tunaloliona kwenye fungu hili? (Kwamba Isaya (nabii wa Mungu) ana ujumbe ambao haukukubaliwa ulimwenguni kote).
      1. Mkono wa Mungu una nini cha kufanya kwa ujumbe huu? Kwa kawaida, watu hunena kupitia kwenye vinywa vyao. Huu ni ujumbe kuhusu uwezo wa Mungu).
    2. Soma Isaya 53:2. Umewahi kujiuliza kwa mshangao kuwa kwa nini Yesu hakuja duniani kama mwanadamu mwenye utukufu au angalao basi kama Mwana wa Mfalme au Mfalme? Hilo lingemfanya aweze kuaminika mara moja/papo hapo. (Yesu alikuja kwa njia isiyo ya kawaida-hii ni kwa mujibu wa mantiki ya kibinadamu. Lakini, hili lilikwishasemwa tayari na Isaya).
    3. Soma Isaya 53:3-5. Unafikiri kwa undani kwa kiasi gani kuwa kuna muungano kati ya maisha ya Yesu na unabii huu? (Unasema kwa dhahiri kabisa kuwa Yesu "alijeruhiwa kwa makosa yetu". Linganisha Yohana 19:18 & 34 kuonyesha kuwa Yesu siyo kwamba tu alijeruhiwa kwa mkuki, bali alisulubiwa-kwa kupigiliwa misumari msalabani).
    4. Soma Isaya 53:6-7. Fungu hili linafananaje/linalinganishwaje na huduma ya patakatifu iliyoelezewa kwenye Agano la Kale? (Linamlinganisha Yesu kwa dhahiri kwamba siyo kirahisi tu ni mwana-kondoo, bali ni yeye yule aliyetumika kwenye kafara za hekaluni kwa sababu fungu hilo linasema kuwa "BWANA ameweka juu yake maovu yetu sisi sote").
    5. Soma Isaya 53:12. Isaya alibashiri nini kuwa Masihi angefanya kwako na kwangu? (Kwamba aliyatoa maisha yake kuichukua dhambi yangu na kuniombea).
      1. Rafiki, je, waweza kutilia mashaka kwamba Yesu ndiye mwana-kondoo aliyezungumziwa katika kitabu cha Isaya-kitabu ambacho dini tatu kubwa duniani zinaamini kuwa ni neno la Mungu?
  2. Imani Yaeleweka
    1. Soma Warumi 5:18-20. Ulifanya nini hadi kusababisha adhabu ya hukumu ya Adamu na Hawa kuwa juu yako? (Kwa kuzaliwa? Fungu linasema kuwa adhabu ya hukumu ilikuwa juu ya "watu wote").
      1. Ulifanya nini hadi kusababisha utii na haki ya Yesu kuwa juu yako? (Kwa kuzaliwa? Fungu linasema kuwa "watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki").
        1. Je, hii inamaanisha kuwa wokovu huja wenyewe?
    2. Soma Warumi 6:1-5. Je, fungu hili linapendekeza kuwa tendo lolote ni muhimu kwa upande wetu kushiriki katika neema tupewayo na Yesu? (Linapendekeza. Linapendekeza  kwamba tunachagua kuingia katika neema kwa "kuzikwa" pamoja na Yesu kwa njia ya ubatizo ili kwamba tuweze kuishi maisha mapya).
      1. Swali linaloulizwa kwenye Warumi 6:1 siyo la kawaida kwa hakika. Kwa nini Paulo hata afikirie kuhusu kuuliza swali kama hilo , hasa ukiangalia mtizamo wake juu ya jambo hili. (Huu ni mojawapo ya ujengaji hoja wenye nguvu kabisa/wa hali ya juu ya kwamba neema huja, tena twaipata si kwa tabia njema. Hitimisho (kutoka Warumi 5) ni la hali ya juu sana kiasi kwamba matendo yetu hayana nafasi yoyote kutupatia wokovu Paulo anahisi analazimika kusema kuwa "Subiri"! Hii haimaanishi kuwa uendelee kutenda dhambi ili neema iendelee kukububujikia!)
      2. Je, hii inaleta maana kwako ukiangalia mustakabali wa mahali patakatifu ulioelezewa kwenye Agano la Kale? Je, mtu aliyeleta kondoo ili achinjwe hekaluni "anastahili" msamaha wa dhambi? Je, mtu huyo "alistahili" haki? (Hapana. Walikuja tu na kafara na kudai faida yake).
    3. Soma Warumi 6:15-17. Ni sababu ipi ambayo inamfanya mfadhili/mtenda wema wa neema anapaswa kumtii Mungu? (Kwa sababu tumemchagua na kuamua kutii mfumo wake).
      1. Fikiria kuhusu suala hili kidogo: kama ungekuwa na mtizamo huu ambao kitabu cha Warumi kimeuelezea, ungeweza kufikiria kanuni/sheria yoyote ya Mungu kuwa kikomo cha uhuru wako?
      2. Kuna kitu ambacho ungependa kukifanya kama "ungesimamisha/ungeahirisha sheria" kwa muda? Mtu ambaye ungependa kufanya naye mapenzi? Kitu ambacho ungependa ukiibe? Tabia ya kibinafsi ambayo ingefanya watu wengine wakuhusudu? Ulipizaji kisasi ambao ungependa kuufanya?
        1. Kama jibu lako kwa lolote kati ya maswali hayo ni "Ndiyo, ningependa kuahirisha sheria kwa mwaka mmoja", jiulize kuwa kwa nini Mungu ana sheria zake? (Shetani anajaribu kuficha ukweli/uhalisia kwamba sheria za Mungu ni kwa ajili ya faida yetu).
        2. Au, je, ni kama tu msukumo wa asili wa mioyo yetu ya kidhambi kutaka kutenda dhambi?
        3. Kama dhambi ni kitu ambacho tungependa kufanya, kama sheria zingeahirishwa/zingesimamishwa kwa muda, kwa nini Yesu aliteseka sana kwa ajili ya dhambi? Kwa nini mwana-kondoo, vivyo hivyo, lazima afe-tena kwa  machungu makubwa? (Hiki ndicho kijalizo cha wimbo (kauntapointi) kwa upendo wa Mungu. Tunadhani ya kwamba dhambi itatuletea furaha, lakini kile ambacho kwa hakika Shetani anakitafakari akilini mwake kwa ajili yetu ni kile alichomtendea Yesu. Kama tu tungeweza kuona kwa makini malengo ya Mungu na malengo ya Shetani, tungeikimbia dhambi).
    4. Soma Warumi 7:1-4. je, tunafungwa na sheria? (Hapana. Haitufungi tena kama vile tusivyofungwa na viapo vyetu vya ndoa pale ambapo mwenza anapofariki.)
      1. Fungu la 4 linamaanisha nini pale linaposema kuwa "Mpate kuwa mali ya mwingine" au "kusudi tumzalie Mungu matunda"?" (Tuna wajibu mpya wa aina fulani).
      2. Kwa wakati huu, je, tunaishi maisha yasiyokuwa na dhambi? (Soma Warumi 7:21-25. Unapaswa kusoma Warumi 7 yote ili kuweza kupata maana sahihi juu ya hili. Paulo anaonekana kusema kuwa hata pale ambapo tupo chini ya neema, tunashindana na dhambi).
        1. Kwa nini kuwepo na ushindani kama sheria imetufia maishani mwetu?
    5. Soma Warumi 8:1-14. Huu ni usomaji mrefu sana, lakini nafikiri ni wa muhimu ili kuweza kuelewa kuhusu neema. Sasa basi ya kwamba hatufungwi na sheria, je, tabia yetu inahusika? Mtizamo wetu unahusika? (Ndiyo! "Kama unaishi kwa mujibu wa asili yako ya dhambi utakufa". Mara Roho Mtakatifu anapotugusa kwamba Mungu alitupenda sana hadi kufa kwa ajili yetu; Mara Roho Mtakatifu anapotugusa kwamba Yesu aliteseka adhabu ya asili kwa ajili ya dhambi zetu-na kwamba tulikufa dhambini ndani ya Yesu; Mara Roho Mtakatifu anapotugusa kwamba sheria ya Mungu ni kwa ajili tu ya faida yetu na kwamba Shetani ana uharibifu tu akilini mwetu, basi tuna matamanio ya kuishi kwa mujibu wa matakwa ya Mungu. Tumetayarisha
      akili zetu kwa kile Roho Mtakatifu anatamani tukifanye).

      1. Utunzaji wa Sabato ni muhimu kiasi gani katika haya maisha mapya? (Wengine watasema kuwa huku ni kujaribu kuishi kwa kufuata sheria. Lakini, sabato inatupatia nguvu upya kuishi maisha yenye kuongozwa na Roho. Inatukumbusha kuwa Yesu aliumba ulimwengu (hivyo kuonyesha mamlaka yake juu yetu), inatukumbusha kuwa aliishi, alikufa na alifufuka kutoka kaburini kwa ajili yetu (hivyo kuonyesha upendo wake na uokolewaji wetu), inatuwekea muda kwa ajili ya sisi kutayarisha akili zetu kwa kile ambacho Roho anatamani).
    6. Rafiki, je, leo hii utautoa mtazamo wako kwa Mungu? Je, utamwomba Roho Mtakatifu akusaidie uweze kutayarisha akili/mawazo yako kwa kile ambacho Mungu anatamani? Je, utaipa kisogo asili
      yako ya dhambi?

  3. Wiki Ijayo: Pumziko.

No comments:

Post a Comment