Tuesday, May 5, 2009

Lessoni Somo la 6: Dhambi

(Mwanzo 3, Warumi 5, 6 & 8)


Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani, Kihispania, Kizulu, nk.

Utangulizi: Tafakari juu ya mwenzi (mke/mume) anayeamua kukuudhi kwa makusudi. (Natumaini hili ni gumu kulitafakari!) Je, mtizamo huo ni kama ule wa upendo? Je, Hili latufundisha chochote kuhusu dhambi au sheria ya Mungu? Baadhi ya wakristo kadhaa hujisumbua wakidai kwamba wanaweza kufanya chochote wanachotaka na wakati huo huo wakiendelea kuwa wafuasi wapenzi wa Kristo. Wanajenga hoja kuwa sheria haifanyi kazi tena, kwa hiyo hakuna haja tena ya kutilia maanani matamanio na maelekezo ya Mungu. Je, hii ni kweli? Je, inaleta maana? Kwa nini Mungu anatupa maelekezo? Hebu tujivinjari ndani ya Biblia zetu na kujaribu kujifunza zaidi juu ya dhambi!

I. Dhambi: Mwanzo Wake Hapa Duniani

A. Soma Mwanzo 2:16-17. Je, Mungu ameelezea mapenzi yake kwa Adamu?

1. Kwa nini Mungu awe na sheria kama hiyo? Kwa nini kulikuwa na haja ya kuwa na sheria zozote katika bustani ile iliyokuwa kamilifu?

2. Unadhani “sheria” ya Mungu illileta maana kwa Adamu? (“Kwa nini Mungu awazuilie wanadamu kuhusu jambo fulani,” yumkini Adamu aliuliza hivyo. Huenda Adamu alifikiri ya kuwa: ‘”Ujuzi ni kitu kizuri, na si kitu kibaya!” “Kwa nini nisiaminike?”)

B. Soma Mwanzo 3:1. Kwa nini Shetani anauliza kuhusu kula matunda ya miti ya bustani? (Hawa "alikosa mkutano wa maelekezo” kuhusu kula matunda ya miti ya bustani. Shetani hahitaji suluhisho la kama Hawa anaelewa sheria ya Mungu).

C. Soma Mwanzo 3:2-3. Je, Hawa anajibu kwa usahihi? (Amejibu uongo na tena kaongeza mkanganyiko. Kama ukirejea Mwanzo 2:16-17 utaona ya kwamba Mungu hakusema chochote kuhusu “kugusa” tunda. Kwa mujibu wa Biblia Mungu alisema tu kuwa “Msiyale”. Na pia, kulikuwa na miti miwili katikati ya bustani: Mti wa Ujuzi wa Mema na Mabaya na Mti wa Uzima. (Mwanzo 2:9)).

1. Je, kujizuia kugusa tunda lilikuwa wazo zuri? (Kama utajizuia kula tunda, itasaidia kama utaepuka kuligusa).

2. Je, Hawa alikuwa akifanya jambo sahihi aliposema kuwa kama angegusa tunda angekufa? (Soma Kumbukumbu la Torati 4:1-2. Tunaanza kufumbuliwa macho kuhusu dhambi. Hawa tayari yupo kwenye matatizo. Ni kosa zito kuchanganya kile ambacho “Mungu amesema” na “wazo zuri” pale linapokuja suala la dhambi. Unapowafundisha wanao, usiwachanganye akili zao juu ya kile ambacho ni dhambi na kile ambacho ni mawazo mazuri ya kuzuia dhambi).

D. Soma Mwanzo 3:4-5. Nyumbulisha asili ya dhambi. Ni kwa jinsi gani dhambi inajiwasilisha kwa wanadamu? (Kwanza, kwa dhahiri kabisa Shetani analeta mgongano na Mungu. Pili, Shetani anapendekeza kuwa Mungu amemdanganya Hawa ili aendelee kubakia dhaifu. Anaweza kuwa kama Mungu).

1. Unawezaje kuelezea jaribu la Shetani kwa Hawa? Je, ni hamu ya chakula? Je, ni imani? Je, ni ulafi? Je, ni ubatili/majisifu? Je, ni majivuno? (Kwa hakika ni majivuno, ubatili/majisifu na upungufu wa uaminifu kwa Mungu).
2. Linganisha Mwanzo 3:22 na Mwanzo 3:5. Je, Shetani alikuwa anasema ukweli? (Kwa sehemu fulani).

E. Soma Mwanzo 3:6. Kwa nini Hawa alikula tunda wakati alijua kile Mungu alichosema? (Fungu linasema kuwa tunda lilikuwa lapendeza macho. Lilionekana kuwa lafaa kwa chakula. Lingempatia ujuzi).

1. Kwa nini muonekano wa tunda uwe kigezo kwenye uamuzi wa Hawa? (Kile alichoona kilikinzana na kile alichotarajia kutoka kwenye mti ambao Mungu alisema kuwa ungesababisha kifo). Kwa hakika “mti wa kifo” ungekuwa na tunda baya, au angalao tunda lenye muonekano wa kushuku).
a. Je, hilo lilikuwa ni fikara la kijuujuu/haraka haraka?

2. Je, dhambi ya Hawa ilianza kwa kukua polepole? (Ndiyo. Ilianza pale alipotafsiri vibaya sheria ya Mungu. (Mwanzo 3:3). Aligusa tunda kabla hajalila. Kwa sababu hakufa pindi alipogusa tunda, aliongozwa kuamini kwamba Mungu hakuwa wa kuaminika (hakuwa mwaminifu) na kwamba angepata maarifa kwa kula tunda. Ndipo alipohitimisha ya kwamba lazima tunda litakuwa zuri tu kwa kuwa lilikuwa la kupendeza).

3. Ni mara ngapi umefikiri ya kwamba Mungu hakuwa mwaminifu pale ambapo tatizo lilikuwa ni kushindwa kwako kusoma na kuelewa neno la Mungu?

F. Soma 1 Timotheo 2:14. Kwa nini Adamu aliingia dhambini? (Paulo hasemi, lakini inaonekana kwa dhahiri kabisa kuwa Adamu alimchagua Hawa badala ya Mungu. Alichagua uumbaji badala ya Muumba).

1. Paulo anaonekana kuhitimisha kwamba Adamu ana haki ya kupata sifa kwa sababu hakudanganywa na Hawa alidanganywa. Unalitazamaje hili? (Dhambi zote ni dhambi, lakini natizama kutokutii kwa makusudi kama mwangaza mbaya zaidi. Fikiria jinsi unavyolinganisha hayo masuala mawili pale ambapo watoto wako wasipokutii).

G. Ni fundisho gani kuhusu dhambi tunalojifunza kutoka kwenye anguko la Adamu na Hawa? (Kwanza, lazima tuwe makini sana pale ambapo mtu yeyote anapopingana na neno la Mungu. Hatuna tumaini la kuwa makini isipokuwa tu tutakuwa tunajua neno la Mungu. Pili, lazima tumwamini Mungu. Ilimpasa Hawa kuridhika na ujuzi ambao Mungu alimpatia. Majivuno/majisifu, uchoyo na kukataa mamlaka ya Mungu ndiko kulisababisha Hawa aanguke dhambini. Tatu, hatupaswi kuruhusu kitu chochote katika uumbaji kichukue nafasi kubwa kwetu kuliko kumtii Mungu. Huu ndio mzizi wa wizi, uzinzi na wivu).

H. Hebu twende mwishoni mwa Biblia. Soma Ufunuo 14:12. Mungu anahitaji nini kwa watu wake mwisho wa wakati? (Kitu kile kile alichokuwa akikihitaji pale mwanzo-uaminifu na utii).


II. Dhambi: Asili yake

A. Hebu tusome tena Mwanzo 3:22. Nilifikiri Mungu aliwaumba wanadamu kwa mfano wake (Mwanzo 1:27). Kuna ubaya gani kwa wanadamu kuujua uovu, ikiwa ni pamoja na kuujua wema kama vile Mungu ajuavyo?
1. Kuna ubaya gani wa “kuujua uovu” na kuishi milele? Mungu anaishi milele!

B. Ni nini kwa hakika ambacho Adamu na Hawa walikipata kimaarifa baada ya kula tunda? Je, tunda lile lilikuwa na dawa ya kuleta ujuzi? (Kamwe tunda halikuwapa ujuzi mpya. Matendo yao ya kutomtii na kutomwamini Mungu ndiyo yalikuwa “ujuzi mpya”. Kitendo hicho kilivunja uhusiano wao na Mungu na kikaweka uhusiano wao na Shetani. Maarifa yote mabaya na ya kutisha ndiyo yaliyofuatia).

1. Hili linapendekeza nini juu ya asili ya dhambi? (Ni kutokuamini na kutokutii kwa sababu tunafikiri ya kwamba tunajua zaidi ya Mungu).

C. Soma Warumi 5:16-17. Matokea ya dhambi ya Adamu na Hawa yalikuwa yapi? (Yalituletea laana/hatia).

1. Kwa nini? (Uhusiano wa mwanadanu na Mungu mkamilifu ulivunjika. Tukawa wadhambi ambao tukaupa utii wetu kwa Shetani).

2. Je, zawadi ya Yesu inatofautianaje na zawadi ya Adamu na Hawa? (Dhambi moja ilileta mpasuko kwenye uhusiano wetu na Mungu na kutuletea laana/hatia. Lakini, maisha, kifo na ufufuo wa Yesu kwa niaba/ajili yetu imefunika dhambi zote zilizofanyika tangu wakati wa Hawa).

D. Soma Warumi 6:11-13. Twajihesabuje kuwa “wafu” kwa dhambi? Je, hilo ni kama vile kurudia jambo la ujuzi wa mabaya? (Adamu na Hawa, kama wangetii, hatimaye wangeelewa kuhusu uovu-walakini wasingekuwa sehemu ya uovu huo. Tunaelewa kuhusu uovu kwa sababu ya Adamu na Hawa (pamoja na maanguko yetu wenyewe), lakini Mungu anatutaka tuishi kana kwamba hatujui uovu. Anatutaka tuwe “wafu” kwa ujuzi huo).


III. Dhambi: Mwanzo Wake Ndani Yetu

A. Je, tunaishije maisha ya kuifia dhambi?

B. Nilimpa Hawa wakati mgumu kwa kusema kuwa “Usiguse” pale ambapo huenda alikuwa anajaribu kuepuka dhambi. Unadhani ni nini ambacho kingekuwa njia salama zaidi kuepuka dhambi ya kula tunda lililokatazwa?

C. Soma Warumi 8:5-8 and Mathayo 5:27-28. Hebu tuangalie hili fungu la pili kidogo. Yesu anaonekana kusema kuwa kuna tatizo kwenye “kuzini nafsini?” Kwa nini hivyo? (Una nia ya kufanya uzinzi, kinachokosekana ni fursa tu. Kama ungekuwa na fursa, ungefanya uzinzi).

1. Je, fungu hilo la Warumi 8 linapendekeza nini kuhusu uhusiano uliopo kati ya akili zetu/mawazo yetu na dhambi? (Linapendekeza kuwa tunaanza na hatua ya kufikiri akilini kabla ya hatua ya kutenda kivitendo. Kile tunachokitenda huagizwa na kile tunachokifikiri. Aidha tutaangalia kile ambacho Mungu anakitaka au tutaangalia matamanio yetu ya kibinafsi).
a. Je, wazo hili “lafananaje” na hali ya Hawa? (Aliamua kutomtii Mungu kabla hajala tunda. Aliamua kutizama matamanio yake ya kichoyo. Paulo anapotuambia kuwa “tufe” kwa dhambi, anamaanisha kuwa tusiishi vivyo katika mawazo yetu. Tusitizamie matamanio yetu ya kibinafsi.

2. Je, unafikiria juu ya dhambi ambazo huzitendi?

a.Kama ndivyo, je, ni kama tu suala la muda kabla hujazitenda?

D. Rafiki, naamini dhambi kwa zaidi ni mtizamo-mtizamo wa ubinafsi. “ujuzi” wa uovu ulikuwa awali ya yote uamuzi wa kutomwamini na kutomtii Mungu. Yesu amekarabati uharibifu uliofanywa na Adamu na Hawa, ila naamini Paulo na Hawa wanatufundisha kuwa uaminifu na utii ni muhimu sana kwenye uhusiano wetu na Mungu. Je, utatubu dhambi zako na kumwomba Mungu kukupatia mtizamo wa uaminifu na utii?


IV. Wiki Ijayo: Neema.

Imetafsiriwa na kuandaliwa na
Mgune Masatu.

1 comment:

  1. Swali 1: Tunatofautishaje kati ya chanzo cha dhambi (kabla na baada ya anguko la Adam na Hawa) na matokeo ya dhambi?

    Swali 2: Kwenye Lesoni hii, tunajadili chanzo cha dhambi au matokeo yake?

    ReplyDelete