Friday, May 29, 2009

Somo la 10: Uanafunzi

Uanafunzi
(1 Wakorintho 12, Kutoka 18, Mathayo 20, Marko 8)
Maisha ya Mkristo: Somo la 10
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sememu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani, Kihispania, Kizulu, nk.

Utangulizi: “Ongoza, fuata au pisha njia” ni msemo wenye sifa ya msingi ya Thomas Paine, “Baba wa Taifa” la Marekani. Kama ningekupa chaguo la hayo matatu, wangapi mngechagua “kufuata?” Nahisi siyo wengi. Wengi hupenda kuongoza ama kwenda njia zao wenyewe. Inamaanisha nini kuwa mfuasi wa Mungu? Je, hii ni aina ya kitamaduni ya mfuasi? Au je, huyu ni mfuasi ambaye pia anaongoza? Hebu tujivinjari katika Biblia na kubaini!

I. Mwili wa Wafuasi

A. Soma 1 Wakorintho 12:27. Je, kuwa sehemu ya mwili wa Kristo ina nini cha kufanya na dhana ya uanafunzi? (Tunapomfuata Yesu, tuna sehemu ya kufanya katika utendaji kazi. Cha kufurahisha zaidi, utendaji kazi wetu kama wanafunzi unalinganishwa na “mwili.”)

B. Soma 1 Wakorintho 12:28. Kati ya majukumu haya, ni yapi ni majukumu ya “kiuongozi” (“Mitume” na “maongozi” yanaonekana kama yanaongoza kiaina.)

1. Wafuasi ni wapi katika kundi hili? (Hilo siyo rahisi kulielezea, si ndiyo? Nadhani “wasaidizi” wanaweza kuwa wafuasi kwa muktadha fulani.)

2. Kwa nini suala la kiongozi na mfuasi ni gumu kulijibu? Kwa nini Mungu ashindwe kuliweka hili dhahiri?

3. Kwa nini Biblia inalinganisha kanisa na mwili badala ya jeshi au taifa? (Kwa sababu msitari kati ya mfuasi na kiongozi hauko wazi sana . Katika jeshi au taifa, kuna viongozi wachache na wengine wote waliosalia hufuata. Lakini, isipokuwa kwa ukweli kwamba Mungu ni kiongozi wetu, kanisa linaonekana kama kitu fulani tofauti kabisa. Nafikiri kwa hakika kabisa hii ndiyo sababu kwamba Mungu alitumia mfano wa mwili badala ya jeshi kuelezea kanisa lake.)

4. Soma 1 Wakorintho 12:20-21. Kanisa linafanyaje kazi pale linapokuja suala la viongozi na wafuasi? (Badala ya mpango wa kiongozi/mfuasi ulio wazi, tunaona juhudi zilizoratibiwa ambapo kila sehemu ni ya msingi. Kila mtu ni muhimu. Kila mtu ana sehemu kubwa sana . Thomas Paine, muasisi wa taifa la Marekani hakuwa na kanisa mawazoni mwake.)

II. Viongozi Wanaojifunza

A. Soma Kutoka 18:13. Je, watu walifurahia hali hii? (Walikuja kwa Musa. Hata hivyo, usemi kwamba “wakasimama kumzunguka….. tangu asubuhi hata jioni” unaweza kuakisi huduma ya polepole.)

1. Je, Musa alifurahia hali hii? (Kazi nzuri iliyoje zaidi ya kuzungumza kwa ajili ya Mungu! Hata hivyo, alifanya kazi kwa saa nyingi.)

B. Soma Kutoka 18:17. Je, haya ni maneno ambayo Musa alitarajia kuyasikia? Je, hakuwa akifanya jukumu kubwa kuzungumza kwa ajili ya Mungu na kulisaidia taifa lake?

C. Soma Kutoka 18:18-23. Je, kama ungekuwa Musa, ungeitikia vipi ushauri wa Yethro (baba mkwe wako)? Ukizingatia kwamba, wewe ndio uliongea na Mungu, na siyo yeye. Kwa nini umsikilize pale ambapo unanena kwa ajili ya Mungu?

1. Gundua (angalia) Kutoka 18:19. Je, Yethro anafafanua kazi ya Musa? (Ndiyo. Anasema kwamba jukumu la Musa lapaswa kuwa kwenda kwa Mungu kwa ajili ya watu, siyo kumuamulia Mungu. Hili ni sahihisho lenye akili. Hii inaashiria kwamba Musa anaelekea kuamini kupita kiasi katika umuhimu wake mwenyewe, wakati ambapo watu wengine wanaweza kufanya kile ambacho Musa anakifanya.)

2. Gundua (angalia) Kutoka 18:23. Je, Yethro anasema nini? (Anasema kwamba Mungu anahitaji kuthibitisha ushauri wake.)

3. Hadi sasa tunajifunza nini kuhusu uanafunzi katika kisa hiki? (Huu ni mfano mwingine wa sheria ya “mwili” ya uongozi-kwamba badala ya kufanya kazi peke yake, Musa anahitaji kuwategemea watu wengine kumsaidia katika jukumu hili muhimu. Jukumu muhimu linahitajika kusambazwa kwa watu wengine wenye uewezo.)

D. Soma Kutoka 18:24-26. Ni kitu gani kizuri tunachojifunza kutoka kwa Musa kama kiongozi? (Kwamba ingawaje anaonekana kupitiwa kidogo na umuhimu-binafsi, anafuata ushauri. Anaonyesha unyenyekevu katika ukubali na utekelezaji wa ushauri mzuri aliopewa.)

1. Hili linatufundisha nini kuhusu taasisi? (Kuendesha taasisi kwa usahihi kunahitaji mpangilio/maandalizi. Kugawanya majukumu, kuchagua watu hodari/wenye ujuzi, na kumuweka Mungu kama kiongozi wa programu ndio ufunguo.)

III. Viongozi Watumishi

A. Soma Mathayo 20:20-21. Kwa kusoma haya mafungu mawili, unafikiri jibu lapaswa kuwa lipi? (Ni aina gani ya viongozi wajao hutuma “mama” kuwafanyia kazi zao za muhimu sana?)

B. Soma Mathayo 20:22. Je, mama ni msanii (mwenye kutoa sauti kana kwamba imetoka kwa mwingine)? Je, hili jibu la “twaweza” ni nini? (Si tu kwamba wanawe wanamtuma mama, bali wanasimama pembeni na kusikiliza mazungumzo!)

1. Unafikiria nini juu ya jibu la wanawe? (Yesu aliwaambia kwamba hawajui kile wanachokiomba, na wao (wangali wakiwa katika dimbwi la upumbavu) wanajibu kuwa “Twaweza.” Viongozi wakamilifu-wadhaifu na mabubu kiasi cha kutosikia!)

C. Soma Mathayo 20:23. Ni nani anayeamua katika uongozi wa kanisa? (Mungu. Yesu anatoa jibu la upole, lakini anaweka wazi kuwa Mungu Baba ndiye atakayefanya maamuzi haya.)

D. Soma Mathayo 20:24. Kwa nini hawakuwa na furaha? Kwa sababu mama zao hawakuwa wenye hamasa vya kutosha? Kwa sababu hawakufikiria kuuliza kwanza? Kwa sababu hawataki kufuata, wanataka kuongoza?

E. Soma Mathayo 20:25-28. Je, Yesu anahitaji mfuasi/kiongozi wa aina gani? (Kiongozi mtumishi. Dhana ya ajabu kiasi gani: kiongozi ambaye anatumia mamlaka kuwasaidia watu wengine, na siyo kujisaidia yeye mwenyewe.)

1. Maneno haya ni yenye mhimili katika historia ya dunia ya sasa. Wanazuoni/watafakari wa siasa wa hali ya juu wa kale Plato na Aristotle,walikuwa na wazo hili kwamba kulikuwa na watu wachache wa hali ya juu ambao wanapaswa kuwa viongozi na wengine waliobaki wanapaswa kuwatumikia kwa ajili ya manufaa mazuri. Yesu anasema kwamba viongozi wanapaswa kuwatumikia watu wao. (“Mtu yeyote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu.”) Ni kutoka katika fundisho hili kwamba tunapata wazo la “mtumishi wa umma” ambalo ni mhimili katika demokrasia ya Marekani.)

2. Somo letu siyo juu ya serikali isiyokuwa na uhusiano wa kidini. Ni nini somo kwa ajili ya uongozi wa kanisa leo?

a. Ni somo gani kwa ajili yako?

IV. Uanafunzi

A. Soma Marko 8:34-38. Je, inamaanisha nini kujitwika msalaba wetu?

1. Soma Mathayo 11:28-30. Nafikiri “nira” ya Yesu kimsingi ni sawa na “msalaba” wake. Inawezaje kuwa “nyepesi” pale ambapo inaonekana kuwa ngumu na ya kutisha/kuogofya? (Kutumikia matakwa yako peke yako inachosha (inaleta uchushaji). Kuwatumikia wengine hufanya maisha kuwa yenye manufaa na yaliyobarikiwa. Inaonekana kana kwamba ni vya kutisha sana kujitoa maisha yetu, lakini Mungu si kwamba anatupatia uzima wa milele kwa mbadilishano huo (mbadilishano mzuri!), bali husaidia wengine katika kuifanya nira “laini”.)

B. Soma Mathayo 7:21. Umewahi kusikia usemi “fimbo kubwa, pasipo ng’ombe?” Unadhani inamaanisha nini? (Mtu anayecheza sehemu ya kuwa mchunga ng’ombe, lakini asiye na ng’ombe-hana kitu.)

1. Je, hicho ndicho Yesu anachokimaanisha hapa? (Inaonekana kwamba Yesu anasema kuwa watu hawa wanaongea tu, hawatendi.)

C. Soma Mathayo 7:22-23. Hebu subiri kidogo, watu hawa wana matendo mengi. Unawezaje kuelezea kwamba Yesu anawakataa wakati wana matendo? (Cha msingi ni kwamba Yesu anasema “ Sikuwajua kamwe.” Mapenzi ya Mungu Baba ni kwamba tumjue Yesu. Hii ndio kazi ya msingi ya mwanafunzi. Kama hatumjui Yesu, basi kazi zetu zimeelekezwa pasipostahili.)

D. Rafiki, je, hii iinakupa picha ya kutosha ya uanafunzi? Mwanafunzi wa kweli anamjua Mungu na pale anapofaa katika kazi ya kanisa. Mwanafunzi wa kweli ana lengo la kusaidia-siyo lengo la kujitukuza nafsi. Kama mtizamo wako si sahihi, je, utamwomba Roho Mtakatifu kuubadilisha leo? Kama haulitumikii kanisa kwa namna fulani, je, utamwomba Mungu kwamba akuonyeshe namna ya kutumikia?

V. Wiki Ijayo: Uwakili.

Imetafsiriwa na kuandaliwa na,
Mgune Masatu.

Friday, May 22, 2009

SOMO LA TISA: MBINGUNI

(2 Wafalme 2 & 13, Mathayo 17, Ufunuo wa Yohana 21)
Maisha ya Mkristo: Somo la 9
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sememu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani, Kihispania, Kizulu, nk.


Utangulizi: Nini kinachokutia hamasa maishani? Pesa, heshima, nguvu/uwezo, upendo. mafanikio, Mungu au yote hayo? Kwa nini nimeorodhesha Mungu kati ya vitia hamasa vya mwanadamu? Kwa sababu Mungu yupo katika mchakato wa uhamasishaji. Kihamasisho kimoja kikubwa ni ahadi yake ya mbingu kwa wale walio waaminifu. Wiki iliyopita nilikuambia utafakari juu ya mkakati wa Shetani pale inapokuja kuhafifisha/kudhoofisha mamlaka ya Mungu. Unadhani ni nini mkakati wa Shetani pale linapokuja suala la mbinguni? Kama mbingu haipo, dhambi (ambayo ipo) inaonekana kuwa nzuri sana, si ndiyo? Angalau mwanzoni. Hebu tujivinjari ndani ya Biblia na kuona kile inachosema kuhusu ujira wetu wa milele!

I. Eliya, Elisha na Mbingu

A. Soma 2 Wafalme 2:1 na 2 Wafalme 2:11-12. Elia alikufaje? (Hakufa!)

1. Alikwenda wapi? (Alikwenda mbinguni moja kwa moja.)

2. Tunajifunza nini kuhusu mbingu kutoka kwenye haya mafungu machache? (Ni “juu” na ina usafiri wa umma (wa watu wote). Kwa dhati zaidi, lazima iwe sehemu halisi ambapo miili ya kawaida inaishi.)

3. Unaelezeaje mwitikio wa Elisha? Kurarua mavazi yako inamaanisha kuwa huna furaha. (Elisha alimwita Eliya “gari la Israeli na wapanda farasi wake.” Israeli haikuwa na magari na wapanda farasi. Elisha alikuwa anasema kuwa Eliya alikuwa nguvu ya Israeli, na alisikitika kumwona akienda.)

B. Soma 2 Wafalme 13:21. Nini kilitokea kwa Elisha pale alipokufa? Je, alifuata nyazo za rafiki yake Eliya? (Hapana. Mifupa yake ilikuwa kaburini.)

1. Je, hii inamaanisha kuwa Elisha hakuwa mbinguni? (Tunajua kwa hakika kwamba, tofauti na Eliya, mwili wake haukuwa mbinguni.)

II. Musa na Mbingu

A. Soma Kumbukumbu la Torati 34:5-7. Nini kilitokea kwa mtu muhimu Musa pale alipokufa? (Mungu alimzika!)

1. Je, Musa alikuwa mbinguni pale alipokufa? (Eliya anatuonyesha kuwa Mungu alikuwa na uchaguzi wa kumpeleka mbinguni, lakini fungu linasema kuwa badala yake Mungu alimzika.)

B. Soma Yuda 1:9. Yuda anaongelea juu ya nini? (Inavyoonekana, baada ya Musa kufariki, Mungu na Shetani walikuwa na malumbano/mgogoro juu ya mwili wa Musa. Katika malumbano hayo, Mungu alimkemea Shetani.)

1. Unafikiri kuwa ni nini kilikuwa kiini cha malumbano/mgogoro? (Bila shaka Mungu aliutaka mwili wa Musa na Shetani hakufikiri kuwa Mungu alikuwa na haki kwa mwili huo kwa sababu Shetani alikuwa “mtawala” wa dunia.)

C. Soma Mathayo 17:1-3. Nani aliyeshinda malumbano/mgogoro juu ya mwili wa Musa? (Mungu alishinda!)

1. Mungu aliupeleka mwili wa Musa wapi? (Lazima itakuwa mbinguni kwa sababu huko ndiko Eliya alikopelekwa!)

2. Mpangilio wa muda wa Musa kwenda mbinguni ulikuwa upi? (Muda fulani baada ya Mungu kuwa amemzika.)

III. Yesu Mbinguni

A. Soma Mathayo 22:23-28. Kwa nini Masadukayo waulize swali hili ikiwa hawakuamini katika ufufuo wa wafu? (Walitaka kuonyesha kuwa hilo lilikuwa wazo lisilokuwa la kivitendo.)

B. Soma Mathayo 22:29-32. Yesu anasema nini kuhusu kama ufufuo uko mbeleni mwako? Yesu anasema nini kuhusu mipango ya Mungu kwa waaminio? (Yesu kwa hakika anaidhinisha wazo la kwamba tutafufuliwa. Analijenga hilo katika Biblia na katika uwezo wa Mungu.)

C. Tunaona kutoka kwenye visa hivi na tamko la Yesu kwamba kuna mbingu na pia kuna ufufuo ujao. Hilo linatufundisha nini kuhusu upendeleo alio nao Mungu ndani yako? (Kwamba Mungu ana mpango wa wokovu kwetu ili kwamba kama tu waaminifu, tunaweza kuishi pamoja naye.)

IV. Lini Mbingu?

A. Kuna uvumi mkubwa na mjadala kuwa nini kinatokea pale mtu anayeamini anapokufa. Wengine wanaamini kuwa “roho” ya mtu inakwenda mbinguni wakati mwili unaoza. Wengine wanaamini kwamba roho haipo tofauti na mwili, na mwili na roho vinakuwa katika hali ya kutokuwa na fahamu kaburini hadi ufufuo. Je, visa vya Eliya, Elisha na Musa vinatufundisha nini kwa hali ya juu kabisa ya uhakika? (Eliya anatufundisha kuwa Mungu anaweza kutuchukua mbinguni moja kwa moja bila kuonja mauti. Elisha anatufundisha kuwa hali ya kawaida ya kifo ni kwamba miili yetu inaoza na kubakia hapa duniani. Musa anatufundisha kuwa mara baada ya kufa, na miili yetu kuzikwa, Yesu anaweza kutufufua na kuturejesha maishani kabla ya ufufuo wa jumla.)

1. Visa hivi vinaelekea kutufundisha nini kuhusu kuwa na roho yenye utambuzi inayojitegemea? (Wana tabia ya kubainisha uongo. Kwa nini mwili wa Eliya ulichukuliwa juu? Kwa nini mwili wa Musa uwe kiini cha mpambano kama tuna roho iliyopo mbinguni? Ukweli kwamba Mungu alikusanya miili ya waaminio maarufu wawili yaelekea kuonyesha kwamba mbinguni tutakuwa na miili yetu. Mungu anaweza kutuchukua mbinguni wakati wowote kipindi cha uhai wetu au baada ya kuwa tumefariki. Lakini, inaonekana kuwa anachukua kila kitu, na anavichukua mbinguni, mahala ambapo miili inaonekana kuwa ya muhimu.)

V. Wewe na Mbingu

A. Kwa hiyo, upo mbinguni na mwili wako wote. Kuna nini pale cha kufanya? Je, kuna sehemu ya maji? Kuna miti ya kukwea? Je, ni nini kuhusu mikahawa mizuri?

B. Soma Ufunuo 21:2-3. Kitu cha kwanza kufanya mbinguni ni nini? (Tutakuwa na uhusiano wa karibu na Mungu. Muumba wetu na Mkombozi wetu-yeye atupendaye upeo (zaidi ya tunavyoweza kufikiria)-atakuwepo.)

C. Soma Ufunuo 21:4. Hali ya hisia zetu itakuwaje mbinguni? (Hatutasikitika. Hapatakuwepo na mauti wala maumivu. “Mambo ya kwanza” kuelekea kaburini yamekwisha kupita.

D. Soma Ufunuo 21:5 na Isaya 65:17. Unapenda mambo mapya? (Yote yatakuwa mapya mbinguni na katika nchi mpya.)

E. Soma Ufunuo 21:10-11 na Ufunuo 21:18-21.
Fikiria kito kizuri sana na cha thamani. Halafu tafakari mji wote unaoonekana kama kito kimoja kikubwa kizuri cha ajabu! Hayo ndiyo maisha yetu ya baadaye!

1. Kwa nini Mungu afanye Yerusalemu mpya kama hivyo? (Muda wa kujitoa/kujikana nafsi umepita. Hii inapendekeza kwamba Mungu huumba na kutupatia dunia kwa ukarimu mkubwa.)

F. Soma Ufunuo 21:23-26. Tunajifunza nini kuhusu masharti ya mwangaza na mwelekeo wa ulalaji?

1. Majadiliano kuhusu “wafalme” na “mataifa” yanapendekeza nini? (Ya kwamba tutakuwa na mpangilio.)

G. Soma Ufunuo 22:1-3. Hili linatuambia nini kuhusu sehemu za maji, ukweaji miti na kula kule mbinguni? (Vyote hivyo vipo huko.)

1. Wazo la ulaji na unywaji huu unapendekeza nini kuhusu uwepo wa roho? (Ya kwamba sisi siyo roho.)

2. Ona tena rejeo la “mataifa.” Mjadala wa Yerusalemu mpya unajumuisha uhalisia wote wa mambo ambao u dhahiri kwetu-isipokuwa utadhihirishwa kwa uzuri zaidi ya tujuavyo. Hili linatufundisha nini kuhusu mbingu? (Ya kwamba itakuwa ya kawaida/yenye kujulikana/zoevu kwetu katika njia nyingi.

H. Ninasoma kitabu kilichoandikwa na Randy Alcorn kinachoitwa "Mbingu." Alcorn anaiangalia Biblia na kuhitimisha kwamba Mungu anapoileta Yerusalemu Mpya hapa duniani iliyofanywa upya, kwamba alama za kiujumla za kijiografia zitaumbwa upya. Ufunuo 21:1 inafunua kuwa bahari haipo tena. Hiyo itapanua ukubwa wa ardhi ya sasa. Kwa hiyo, uelewa wa Alcorn unakubalika. Ningependa kuendelea kuishi Virginia . Je, ungependa, katika nchi mpya, kuishi pale unapoishi kwa sasa? Kuweza kutembelea mahala pale ulipokulia?

I. Soma Yohana 14:2-3. Oh Hapana! Je, sasa tumepunguziwa hadi kubakiwa na “chumba” kule mbinguni? (Hapana. Hii ni “Yerusalemu Mpya” tunayoimiliki. Katika Yerusalemu Mpya kuna sehemu yenye ukomo. Tuna umiliki wetu katika Yerusalemu na nchi zetu za nyumbani popote pale tunapotaka.)

1. Soma Isaya 65:21-22. Je, hii ni nchi ya nyumbani ambayo nimeirejea hivi punde? (Sina hakika na jinsi ya kushughulika na hili fungu. Nafikiri kimsingi linarejea mpango wa Mungu kwa Wayahudi kama wangekuwa waaminifu kwake. Hata hivyo, jinsi baadhi ya unabii ulivyo na utimilizwaji zaidi ya mmoja, nadhani hili laweza kuwa sahihi kabisa (kwa kiwango fulani) kujielekeza mbinguni pia. Kwa hakika inatupatia mtazamo ambao Mungu anautaka kwa ajili yetu.)

J. Rafiki, ungependa kuishi milele katika sehemu nzuri na isiyo na kasoro? Sehemu ya furaha? Sehemu nzuri kupita kiasi? Mungu amewaahidi watu wake mbingu, Yerusalemu Mpya na nchi mpya. Waweza kuwepo. Utatubu dhambi zako kwa Mungu, kuyakubali maisha na kifo cha Yesu kwa niaba yako, na kumwomba Yesu kuungana naye katika ule ufufuo wenye utukufu katika maisha mapya pamoja naye?

VI. Wiki Ijayo: Uanafunzi.

Sunday, May 17, 2009

Lesoni Somo la 8: Pumziko


(Kutoka 20, Mathayo 5, Wakolosai 2, Waebrania 4)

Maisha ya Mkristo: Somo la 8

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sememu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani, Kihispania, Kizulu, nk.

 
 

Utangulizi: Kama kuna kitu kinahitajika kufanyika, nataka kukifanya sasa hivi. Kama una furaha kama mimi, basi pumziko la "uhuru wa hatia" ni la thamani kubwa. Hiyo ndiyo maana ninaipenda sana Sabato. Nafahamu kwamba sitakiwi kufanya kazi siku ya Sabato, kwa hiyo naweza kupumzika pasipo kujisikia hatia. Wakati nikiwa katika mafunzo ya uanasheria, kilikuwa kipindi kizuri sana. Marafiki zangu wa dhati walikuwa wakisoma kila siku ili waweze kupata alama nzuri na kufaulu kwa madaraja ya juu. Sikusoma sheria siku ya Sabato na nilibarikiwa kwa hilo. Hebu tujivinjari ndani ya Biblia ili tuweze kubaini kuwa kwa nini pumziko la Sabato bado ni sehemu muhimu ya mpango wa Mungu kwa ajili yetu!

 
 

       I.            Madhumini ya Sabato

                             A.            Soma Kutoka 20:8-11. Mungu anatoa sababu gani kwa ajili ya kuitunza Sabato? (Kwa kukumbuka ukweli kwamba aliziumba mbingu na nchi.)

 
 

  1. Soma Mwanzo 2:2-3. Pale Mungu alipoumba Sabato kwanza, kusudi lake lilikuwa ni nini? (Sababu ile ile iliyoelezewa katika kitabu cha Kutoka-kwa sababu aliuumba ulimwengu.)

                                 C.            Hebu jaribu kujiweka katika nafasi ya Mungu. Mara kwa mara huwa tunasema ya kwamba kwa nini sisi, kama wanadamu, tumfuate Mungu. Ni nini mtazamo wa Mungu juu ya hili? Kama ungekuwa Mungu na uulizwe ya kwamba kwa nini wanadamu wakutumikie, ungesemaje? (Kwa sababu Niliwaumba!)

      1.            Je, hiki ndicho kwa hakika ambacho Mungu anakisema? (Soma Mwanzo 1:1. Hili ndilo tamko la Mungu la kwanza kwetu-ya kwamba yeye ni Muumba.)

     
     

    1. Soma Ufunuo 14:6-7. Tumeangalia madai ya Mungu ya kuabudu katika kitabu cha kwanza cha Biblia. Mungu anatoa sababu gani katika kitabu cha mwisho cha Biblia? (Sababu ya kumwabudu Mungu ni kwa sababu yeye ni Muumba wetu. Kwa hakika, hii inaitwa "injili ya milele".)
    2. Orodha ya Naves namba 104 mafungu ya Biblia chini ya "Muumba," ambapo Mungu aidha moja kwa moja au kupitia kwa wanadamu, anaweka dau madai yake kwa mamlaka juu ya wanadamu katika ukweli wa Uumbaji wake.)
  2. Muda wa mkakati. Kama ungekuwa Shetani, na ungekuwa katika shindano na Mungu juu ya mamlaka kwa wanadamu, lengo lako lingekuwa nini? (Kuhafifisha au kondoa kabisa msingi wa madai ya Mungu ya mamlaka.)
    1. Je, tunaona hili likitokea: je, historia na ukumbusho wa madai ya Mungu ya mamlaka yamemomonyolewa?
    2. Je, mmomonyoko huu wapaswa kuwa na maana yoyote kwa Wakristo? (Martin Luther alisema: " Kama nikitamka kwa sauti kubwa kabisa … kila sehemu ya Neno la Mungu isipokuwa kwa usahihi kwamba sehemu ndogo ambayo dunia na mwovu wanashambulia kwa wakati huo, simkiri Kristo….pale ambapo pambano linapopamba moto, hapo ndipo uaminifu wa askari unajaribiwa.")
      1. Wengi wanasema kuwa Sabato si ya maana tena. Kama Martin Luther yuko sahihi, je, Sabato haipo katikati ya pambano kati ya Yesu na Mwovu?
      2. Kama ipo katikati, je, "tunamkiri Kristo" kama tunashindwa kuchukua msimamo thabiti kwa kukumbuka mamlaka ya Mungu kwa wanadamu kila wiki?

Sabato, Bado ni Sehemu ya Mpango wa Mungu?

  1. Wiki iliyopita tulijadili juu ya "Neema," na kugundua (Warumi 8:2) kwamba "sheria ya Roho wa uzima imeniacha huru mbali na sheria ya dhambi na mauti." Je, hiyo inamaanisha kuwa Amri Kumi (ikijumuisha amri ya Sabato) zimekufa?
  2. Soma Mathayo 5:17-19. Yesu anasema nini katika lengo lake la kuja duniani? (Siyo kufuta/kukomesha Amri Kumi! Bali , alikuja "kuzitimiliza." Lazima nisiwafundishe wengine kuzivunja amri.)
    1. Je, hiyo inamaanisha nini-kutimiliza? (Tulijifunza wiki iliyopita kwamba Yesu alikuja na kufaulu pale ambapo Adamu alishindwa-katika kutunza sheria za Mungu. Lakini, tulijifunza pia kuwa hii siyo leseni (Warumi 6:1) ya kutenda dhambi na kwamba tunatakiwa kuishi maisha "kwa mujibu wa Roho." Warumi 8:5. Hili liko sawa na kauli ya Yesu kwamba kamwe tusimfundishe mtu yeyote kuvunja amri.)
  3. Soma Wakolosai 2:16-17. Hadi hapa tumeshaona kwamba Sabato ipo katikati ya mkwaruzano/ugomvi/pambano na Shetani kwa sababu ni kielelezo cha mamlaka ya Mungu kama Muumba wetu. Je, hapa Paulo anasema kwamba Sabato si kitu? Je, Paulo atakuwa "mdogo" katika ufalme wa mbinguni? (Paulo anaonekana kunukuu kwa harakaharaka kutoka katika kitabu cha Hosea 2:11. Hapo, marejeo ni kwa sikukuu za Kiyahudi ambazo pia ziliitwa kuwa "Sabato." Kwa hakika, neno la Kiyunani liitwalo "Sabato" katika Wakolosai 2:16 ni wingi kwa hakika: "Sabato." Tafsiri nyingi (lakini siyo ya New International Version) zinatafsiri neno "Sabato.")
    1. Paulo anamaanisha nini kwa kuziita Sabato "kivuli cha mambo yajayo?" (Tangu Yesu atimilize huduma za patakatifu za Agano la Kale,inafuata kimantiki kwamba sikukuu za Sabato za Wayahudi, ambazo zilikuwa sehemu ya mfumo wa kafara, zilitimilizwa. Hii haikuwa kweli kwa Sabato ya kila wiki ambayo ilikuwa ukumbusho wa uumbaji, na siyo sehemu ya huduma za patakatifu.)
    2. Wachambuzi wengi wa Biblia, hususan wale wa kale, wanakubaliana na hoja yangu kwamba Wakolosai 2 hairejei Sabato ya kila wiki. Chukulia kile ambacho nukuu za Barners zinasema kuhusu fungu hili (na hili ni mfano hasa wa mengine). Kwanza anatabanaisha kuwa neno hilo ni wingi na kwa hiyo inarejea kwenye sikukuu za Kiyahudi, halafu anaendelea: "Hakuna sehemu ya sheria ya maadili-hakuna hata moja ya amri kumi ingeweza kuongelewa kama 'kivuli cha mambo yajayo.' Kutokana na asili ya sheria za maadili, amri hizi zinawajibika milele na kila mahali.")
  4. Soma Waebrania 4:8-11. Miaka ya hivi karibuni baadhi ya watu wameanza kujenga hoja kuwa tangu ufufuo tumeingia katika wakati wa "Sabato." Kila siku ni Sabato. Ni nini ambacho kingekuwa matokeo ya kimantiki ya hiyo hoja? (Aidha usingeabudu katika siku yoyote au ungeabudu katika siku yoyote.)
    1. Kitabu cha Waebrania kinapendekeza nini kuhusu muda wa kawaida wa kukutana kumwabudu Mungu? (Soma Waebrania 10:25. Inatuambia kuwa yatupasa kukutana pamoja mara kwa mara.)
    2. Kama ungekuwa unasheherekea kuishi katika "wakati wa Sabato," na ukafikiria kuwa unapaswa kukutana mara kwa mara kumwabudu Muumba wako, ni siku ipi ambayo kimantiki ungeichagua? (Soma tena Waebrania 4:9-10. Kama sisi ni wa kuingia katika pumziko la Mungu, kama jinsi Mungu alivyofanya, tungeabudu siku ya Jumamosi! Hili ndilo hitimisho la pekee linaloleta mantiki.)
  5. Wengine wanajenga hoja, ambayo haijengwi kwenye amri yoyote kutoka kwa Mungu inayopatikana kwenye Biblia, kwamba ufufuo wa Yesu siku ya Jumapili ulibadilisha kila kitu kuhusu Sabato. Je, wafuasi wa Yesu wana sababu yoyote ya kufikiri kwamba hiyo ni kweli?
    1. Yesu alisulubiwa siku gani? (Soma Marko 15:42-44. Ijumaa.)
    2. Soma Mathayo 27:50-52. Je, kuna sababu yoyote kwa nini Yesu asingefufuka papo hapo, na katika ushuhuda wa macho ya waliokuwepo ajitoe msalabani kwa kutumia uwezo mkubwa kabisa na utukufu uwe kwa Baba yake?
      1. Wewe, ukiwa kama mzazi, ukimwona mwanao akiteswa na kupigwa, je, usingetaka kumwokoa mara moja?
      2. Wewe, ukiwa kama mzazi, ukimwona mwanao akishinda mpambano wa muhimu sana ulimwenguni, ungependa kusubiri kidogo, tena si siku nzima kumkumbatia kwa kumpongeza na kumpa hongera?
      3. Kwa nini Yesu alisubiri? Dhidi ya silika zote za asili, kwa nini Yesu na Baba walisubiri? (Yesu alipumzika siku ya Sabato kwa sababu ile ile aliyopumzika siku ya Sabato baada ya kuumba ulimwengu. Alikuwa anakumbukia kazi yake halisi/ya awali ya uumbaji na sasa kazi yake ya mwisho kabisa ya kuuokoa uumbaji wake dhidi ya uharibifu.)

Kuitunza Sabato

  1. Kwa mwangaza wa historia ya msingi wake, ni kwa jinsi gani utaitunza Sabato? (Ni siku ya kuachana na kazi na mambo yote ya dunia na kumsheherekea Muumba na Mkombozi wetu! Ni siku maalum ya kusifu na kuabudu.)
  2. Soma Marko 2:23-28. Je, hapa Yesu anasema kwamba kwa kuwa Daudi alivunja sheria ya mkate iliyowekwa wakfu, wanafunzi wake wanaweza kuvunja sheria ya usifanye kazi siku ya Sabato? (Hapana. Yesu anasema kwamba Sabato ilikusudiwa kwa ajili ya matumizi mazuri ya mwanadamu. Mbaraka wa wanadamu, siyo sheria na kanuni zisizo na msingi/sizizo na umuhimu, ndio madhumuni/makusudi ya kufaa ya Sabato.)
  3. Rafiki, unasimama wapi katika pambano dhidi ya mamlaka ya Mungu? Je, u askari mwaminifu na mtiifu kwenye masuala yenye mabishano? Kama siyo, unakosa mojawapo ya mibaraka mikubwa ya Mungu kwa ajili ya wanadamu! Kwa nini usidhamirie sasa hivi kuwa mwaminifu na ubarikiwe pale linapokuja suala la Sabato?

Wiki Ijayo: Mbingu.


 


 

Wednesday, May 13, 2009

Lesoni somo la 7: Neema

Neema
(Isaya 53, Warumi 5-7)

Maisha ya Mkristo: Somo la 7

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sememu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani, Kihispania, Kizulu, nk.

 
 

Utangulizi: pale ambapo rafiki yangu wa Kiebrania alipokuwa akijadiliana nami kuhusu dini, alidai ya kwamba wakristo "wemeteka nyara" dini yake. Katika kumjibu, nilisema kuwa "tumekamilisha" dini yake. Katika kujenga hoja yenye kuleta mantiki, nikamuuliza kuwa huduma ya mahali patakatifu na kutolewa kafara kwa mwana-kondoo, yote hiyo ni juu ya nini? Kama ilikuwa tu ni juu ya kuchinja wanyama ili kutuondolea dhambi, je, ni kwa nini sasa tusiendelee na utamaduni huu? Sio lazima kuwa na kafara hekaluni! Hebu tafakari juu ya hili: Judaism (dini ya Kiyahudi), Uislam na Ukristo, zote hizi hukubali neno la Mungu kutoka katika Agano la Kale, lakini ni Ukristo peke yake unaokamilisha mantiki inayounganishwa na neema. Yesu, mwana-kondoo wa Mungu, anazichukua dhambi zetu. Hicho ndicho kile inachokizungumzia. Hebu tujivinjari kwenye somo letu la neema tuweze kujifunza zaidi!

  1. Neema Yatabiriwa
    1. Siku za hivi karibuni, nilikuwa na watu kadhaa waliokuwa wanapendekeza kwangu kuwa muungano kati ya Yesu na manabii wa Agano la Kale ni mdhaifu. Hebu tuchunguze hili kwa kusoma Isaya 53. Soma Isaya 53:1. Kuna tatizo gani tunaloliona kwenye fungu hili? (Kwamba Isaya (nabii wa Mungu) ana ujumbe ambao haukukubaliwa ulimwenguni kote).
      1. Mkono wa Mungu una nini cha kufanya kwa ujumbe huu? Kwa kawaida, watu hunena kupitia kwenye vinywa vyao. Huu ni ujumbe kuhusu uwezo wa Mungu).
    2. Soma Isaya 53:2. Umewahi kujiuliza kwa mshangao kuwa kwa nini Yesu hakuja duniani kama mwanadamu mwenye utukufu au angalao basi kama Mwana wa Mfalme au Mfalme? Hilo lingemfanya aweze kuaminika mara moja/papo hapo. (Yesu alikuja kwa njia isiyo ya kawaida-hii ni kwa mujibu wa mantiki ya kibinadamu. Lakini, hili lilikwishasemwa tayari na Isaya).
    3. Soma Isaya 53:3-5. Unafikiri kwa undani kwa kiasi gani kuwa kuna muungano kati ya maisha ya Yesu na unabii huu? (Unasema kwa dhahiri kabisa kuwa Yesu "alijeruhiwa kwa makosa yetu". Linganisha Yohana 19:18 & 34 kuonyesha kuwa Yesu siyo kwamba tu alijeruhiwa kwa mkuki, bali alisulubiwa-kwa kupigiliwa misumari msalabani).
    4. Soma Isaya 53:6-7. Fungu hili linafananaje/linalinganishwaje na huduma ya patakatifu iliyoelezewa kwenye Agano la Kale? (Linamlinganisha Yesu kwa dhahiri kwamba siyo kirahisi tu ni mwana-kondoo, bali ni yeye yule aliyetumika kwenye kafara za hekaluni kwa sababu fungu hilo linasema kuwa "BWANA ameweka juu yake maovu yetu sisi sote").
    5. Soma Isaya 53:12. Isaya alibashiri nini kuwa Masihi angefanya kwako na kwangu? (Kwamba aliyatoa maisha yake kuichukua dhambi yangu na kuniombea).
      1. Rafiki, je, waweza kutilia mashaka kwamba Yesu ndiye mwana-kondoo aliyezungumziwa katika kitabu cha Isaya-kitabu ambacho dini tatu kubwa duniani zinaamini kuwa ni neno la Mungu?
  2. Imani Yaeleweka
    1. Soma Warumi 5:18-20. Ulifanya nini hadi kusababisha adhabu ya hukumu ya Adamu na Hawa kuwa juu yako? (Kwa kuzaliwa? Fungu linasema kuwa adhabu ya hukumu ilikuwa juu ya "watu wote").
      1. Ulifanya nini hadi kusababisha utii na haki ya Yesu kuwa juu yako? (Kwa kuzaliwa? Fungu linasema kuwa "watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki").
        1. Je, hii inamaanisha kuwa wokovu huja wenyewe?
    2. Soma Warumi 6:1-5. Je, fungu hili linapendekeza kuwa tendo lolote ni muhimu kwa upande wetu kushiriki katika neema tupewayo na Yesu? (Linapendekeza. Linapendekeza  kwamba tunachagua kuingia katika neema kwa "kuzikwa" pamoja na Yesu kwa njia ya ubatizo ili kwamba tuweze kuishi maisha mapya).
      1. Swali linaloulizwa kwenye Warumi 6:1 siyo la kawaida kwa hakika. Kwa nini Paulo hata afikirie kuhusu kuuliza swali kama hilo , hasa ukiangalia mtizamo wake juu ya jambo hili. (Huu ni mojawapo ya ujengaji hoja wenye nguvu kabisa/wa hali ya juu ya kwamba neema huja, tena twaipata si kwa tabia njema. Hitimisho (kutoka Warumi 5) ni la hali ya juu sana kiasi kwamba matendo yetu hayana nafasi yoyote kutupatia wokovu Paulo anahisi analazimika kusema kuwa "Subiri"! Hii haimaanishi kuwa uendelee kutenda dhambi ili neema iendelee kukububujikia!)
      2. Je, hii inaleta maana kwako ukiangalia mustakabali wa mahali patakatifu ulioelezewa kwenye Agano la Kale? Je, mtu aliyeleta kondoo ili achinjwe hekaluni "anastahili" msamaha wa dhambi? Je, mtu huyo "alistahili" haki? (Hapana. Walikuja tu na kafara na kudai faida yake).
    3. Soma Warumi 6:15-17. Ni sababu ipi ambayo inamfanya mfadhili/mtenda wema wa neema anapaswa kumtii Mungu? (Kwa sababu tumemchagua na kuamua kutii mfumo wake).
      1. Fikiria kuhusu suala hili kidogo: kama ungekuwa na mtizamo huu ambao kitabu cha Warumi kimeuelezea, ungeweza kufikiria kanuni/sheria yoyote ya Mungu kuwa kikomo cha uhuru wako?
      2. Kuna kitu ambacho ungependa kukifanya kama "ungesimamisha/ungeahirisha sheria" kwa muda? Mtu ambaye ungependa kufanya naye mapenzi? Kitu ambacho ungependa ukiibe? Tabia ya kibinafsi ambayo ingefanya watu wengine wakuhusudu? Ulipizaji kisasi ambao ungependa kuufanya?
        1. Kama jibu lako kwa lolote kati ya maswali hayo ni "Ndiyo, ningependa kuahirisha sheria kwa mwaka mmoja", jiulize kuwa kwa nini Mungu ana sheria zake? (Shetani anajaribu kuficha ukweli/uhalisia kwamba sheria za Mungu ni kwa ajili ya faida yetu).
        2. Au, je, ni kama tu msukumo wa asili wa mioyo yetu ya kidhambi kutaka kutenda dhambi?
        3. Kama dhambi ni kitu ambacho tungependa kufanya, kama sheria zingeahirishwa/zingesimamishwa kwa muda, kwa nini Yesu aliteseka sana kwa ajili ya dhambi? Kwa nini mwana-kondoo, vivyo hivyo, lazima afe-tena kwa  machungu makubwa? (Hiki ndicho kijalizo cha wimbo (kauntapointi) kwa upendo wa Mungu. Tunadhani ya kwamba dhambi itatuletea furaha, lakini kile ambacho kwa hakika Shetani anakitafakari akilini mwake kwa ajili yetu ni kile alichomtendea Yesu. Kama tu tungeweza kuona kwa makini malengo ya Mungu na malengo ya Shetani, tungeikimbia dhambi).
    4. Soma Warumi 7:1-4. je, tunafungwa na sheria? (Hapana. Haitufungi tena kama vile tusivyofungwa na viapo vyetu vya ndoa pale ambapo mwenza anapofariki.)
      1. Fungu la 4 linamaanisha nini pale linaposema kuwa "Mpate kuwa mali ya mwingine" au "kusudi tumzalie Mungu matunda"?" (Tuna wajibu mpya wa aina fulani).
      2. Kwa wakati huu, je, tunaishi maisha yasiyokuwa na dhambi? (Soma Warumi 7:21-25. Unapaswa kusoma Warumi 7 yote ili kuweza kupata maana sahihi juu ya hili. Paulo anaonekana kusema kuwa hata pale ambapo tupo chini ya neema, tunashindana na dhambi).
        1. Kwa nini kuwepo na ushindani kama sheria imetufia maishani mwetu?
    5. Soma Warumi 8:1-14. Huu ni usomaji mrefu sana, lakini nafikiri ni wa muhimu ili kuweza kuelewa kuhusu neema. Sasa basi ya kwamba hatufungwi na sheria, je, tabia yetu inahusika? Mtizamo wetu unahusika? (Ndiyo! "Kama unaishi kwa mujibu wa asili yako ya dhambi utakufa". Mara Roho Mtakatifu anapotugusa kwamba Mungu alitupenda sana hadi kufa kwa ajili yetu; Mara Roho Mtakatifu anapotugusa kwamba Yesu aliteseka adhabu ya asili kwa ajili ya dhambi zetu-na kwamba tulikufa dhambini ndani ya Yesu; Mara Roho Mtakatifu anapotugusa kwamba sheria ya Mungu ni kwa ajili tu ya faida yetu na kwamba Shetani ana uharibifu tu akilini mwetu, basi tuna matamanio ya kuishi kwa mujibu wa matakwa ya Mungu. Tumetayarisha
      akili zetu kwa kile Roho Mtakatifu anatamani tukifanye).

      1. Utunzaji wa Sabato ni muhimu kiasi gani katika haya maisha mapya? (Wengine watasema kuwa huku ni kujaribu kuishi kwa kufuata sheria. Lakini, sabato inatupatia nguvu upya kuishi maisha yenye kuongozwa na Roho. Inatukumbusha kuwa Yesu aliumba ulimwengu (hivyo kuonyesha mamlaka yake juu yetu), inatukumbusha kuwa aliishi, alikufa na alifufuka kutoka kaburini kwa ajili yetu (hivyo kuonyesha upendo wake na uokolewaji wetu), inatuwekea muda kwa ajili ya sisi kutayarisha akili zetu kwa kile ambacho Roho anatamani).
    6. Rafiki, je, leo hii utautoa mtazamo wako kwa Mungu? Je, utamwomba Roho Mtakatifu akusaidie uweze kutayarisha akili/mawazo yako kwa kile ambacho Mungu anatamani? Je, utaipa kisogo asili
      yako ya dhambi?

  3. Wiki Ijayo: Pumziko.

Tuesday, May 5, 2009

Lessoni Somo la 6: Dhambi

(Mwanzo 3, Warumi 5, 6 & 8)


Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani, Kihispania, Kizulu, nk.

Utangulizi: Tafakari juu ya mwenzi (mke/mume) anayeamua kukuudhi kwa makusudi. (Natumaini hili ni gumu kulitafakari!) Je, mtizamo huo ni kama ule wa upendo? Je, Hili latufundisha chochote kuhusu dhambi au sheria ya Mungu? Baadhi ya wakristo kadhaa hujisumbua wakidai kwamba wanaweza kufanya chochote wanachotaka na wakati huo huo wakiendelea kuwa wafuasi wapenzi wa Kristo. Wanajenga hoja kuwa sheria haifanyi kazi tena, kwa hiyo hakuna haja tena ya kutilia maanani matamanio na maelekezo ya Mungu. Je, hii ni kweli? Je, inaleta maana? Kwa nini Mungu anatupa maelekezo? Hebu tujivinjari ndani ya Biblia zetu na kujaribu kujifunza zaidi juu ya dhambi!

I. Dhambi: Mwanzo Wake Hapa Duniani

A. Soma Mwanzo 2:16-17. Je, Mungu ameelezea mapenzi yake kwa Adamu?

1. Kwa nini Mungu awe na sheria kama hiyo? Kwa nini kulikuwa na haja ya kuwa na sheria zozote katika bustani ile iliyokuwa kamilifu?

2. Unadhani “sheria” ya Mungu illileta maana kwa Adamu? (“Kwa nini Mungu awazuilie wanadamu kuhusu jambo fulani,” yumkini Adamu aliuliza hivyo. Huenda Adamu alifikiri ya kuwa: ‘”Ujuzi ni kitu kizuri, na si kitu kibaya!” “Kwa nini nisiaminike?”)

B. Soma Mwanzo 3:1. Kwa nini Shetani anauliza kuhusu kula matunda ya miti ya bustani? (Hawa "alikosa mkutano wa maelekezo” kuhusu kula matunda ya miti ya bustani. Shetani hahitaji suluhisho la kama Hawa anaelewa sheria ya Mungu).

C. Soma Mwanzo 3:2-3. Je, Hawa anajibu kwa usahihi? (Amejibu uongo na tena kaongeza mkanganyiko. Kama ukirejea Mwanzo 2:16-17 utaona ya kwamba Mungu hakusema chochote kuhusu “kugusa” tunda. Kwa mujibu wa Biblia Mungu alisema tu kuwa “Msiyale”. Na pia, kulikuwa na miti miwili katikati ya bustani: Mti wa Ujuzi wa Mema na Mabaya na Mti wa Uzima. (Mwanzo 2:9)).

1. Je, kujizuia kugusa tunda lilikuwa wazo zuri? (Kama utajizuia kula tunda, itasaidia kama utaepuka kuligusa).

2. Je, Hawa alikuwa akifanya jambo sahihi aliposema kuwa kama angegusa tunda angekufa? (Soma Kumbukumbu la Torati 4:1-2. Tunaanza kufumbuliwa macho kuhusu dhambi. Hawa tayari yupo kwenye matatizo. Ni kosa zito kuchanganya kile ambacho “Mungu amesema” na “wazo zuri” pale linapokuja suala la dhambi. Unapowafundisha wanao, usiwachanganye akili zao juu ya kile ambacho ni dhambi na kile ambacho ni mawazo mazuri ya kuzuia dhambi).

D. Soma Mwanzo 3:4-5. Nyumbulisha asili ya dhambi. Ni kwa jinsi gani dhambi inajiwasilisha kwa wanadamu? (Kwanza, kwa dhahiri kabisa Shetani analeta mgongano na Mungu. Pili, Shetani anapendekeza kuwa Mungu amemdanganya Hawa ili aendelee kubakia dhaifu. Anaweza kuwa kama Mungu).

1. Unawezaje kuelezea jaribu la Shetani kwa Hawa? Je, ni hamu ya chakula? Je, ni imani? Je, ni ulafi? Je, ni ubatili/majisifu? Je, ni majivuno? (Kwa hakika ni majivuno, ubatili/majisifu na upungufu wa uaminifu kwa Mungu).
2. Linganisha Mwanzo 3:22 na Mwanzo 3:5. Je, Shetani alikuwa anasema ukweli? (Kwa sehemu fulani).

E. Soma Mwanzo 3:6. Kwa nini Hawa alikula tunda wakati alijua kile Mungu alichosema? (Fungu linasema kuwa tunda lilikuwa lapendeza macho. Lilionekana kuwa lafaa kwa chakula. Lingempatia ujuzi).

1. Kwa nini muonekano wa tunda uwe kigezo kwenye uamuzi wa Hawa? (Kile alichoona kilikinzana na kile alichotarajia kutoka kwenye mti ambao Mungu alisema kuwa ungesababisha kifo). Kwa hakika “mti wa kifo” ungekuwa na tunda baya, au angalao tunda lenye muonekano wa kushuku).
a. Je, hilo lilikuwa ni fikara la kijuujuu/haraka haraka?

2. Je, dhambi ya Hawa ilianza kwa kukua polepole? (Ndiyo. Ilianza pale alipotafsiri vibaya sheria ya Mungu. (Mwanzo 3:3). Aligusa tunda kabla hajalila. Kwa sababu hakufa pindi alipogusa tunda, aliongozwa kuamini kwamba Mungu hakuwa wa kuaminika (hakuwa mwaminifu) na kwamba angepata maarifa kwa kula tunda. Ndipo alipohitimisha ya kwamba lazima tunda litakuwa zuri tu kwa kuwa lilikuwa la kupendeza).

3. Ni mara ngapi umefikiri ya kwamba Mungu hakuwa mwaminifu pale ambapo tatizo lilikuwa ni kushindwa kwako kusoma na kuelewa neno la Mungu?

F. Soma 1 Timotheo 2:14. Kwa nini Adamu aliingia dhambini? (Paulo hasemi, lakini inaonekana kwa dhahiri kabisa kuwa Adamu alimchagua Hawa badala ya Mungu. Alichagua uumbaji badala ya Muumba).

1. Paulo anaonekana kuhitimisha kwamba Adamu ana haki ya kupata sifa kwa sababu hakudanganywa na Hawa alidanganywa. Unalitazamaje hili? (Dhambi zote ni dhambi, lakini natizama kutokutii kwa makusudi kama mwangaza mbaya zaidi. Fikiria jinsi unavyolinganisha hayo masuala mawili pale ambapo watoto wako wasipokutii).

G. Ni fundisho gani kuhusu dhambi tunalojifunza kutoka kwenye anguko la Adamu na Hawa? (Kwanza, lazima tuwe makini sana pale ambapo mtu yeyote anapopingana na neno la Mungu. Hatuna tumaini la kuwa makini isipokuwa tu tutakuwa tunajua neno la Mungu. Pili, lazima tumwamini Mungu. Ilimpasa Hawa kuridhika na ujuzi ambao Mungu alimpatia. Majivuno/majisifu, uchoyo na kukataa mamlaka ya Mungu ndiko kulisababisha Hawa aanguke dhambini. Tatu, hatupaswi kuruhusu kitu chochote katika uumbaji kichukue nafasi kubwa kwetu kuliko kumtii Mungu. Huu ndio mzizi wa wizi, uzinzi na wivu).

H. Hebu twende mwishoni mwa Biblia. Soma Ufunuo 14:12. Mungu anahitaji nini kwa watu wake mwisho wa wakati? (Kitu kile kile alichokuwa akikihitaji pale mwanzo-uaminifu na utii).


II. Dhambi: Asili yake

A. Hebu tusome tena Mwanzo 3:22. Nilifikiri Mungu aliwaumba wanadamu kwa mfano wake (Mwanzo 1:27). Kuna ubaya gani kwa wanadamu kuujua uovu, ikiwa ni pamoja na kuujua wema kama vile Mungu ajuavyo?
1. Kuna ubaya gani wa “kuujua uovu” na kuishi milele? Mungu anaishi milele!

B. Ni nini kwa hakika ambacho Adamu na Hawa walikipata kimaarifa baada ya kula tunda? Je, tunda lile lilikuwa na dawa ya kuleta ujuzi? (Kamwe tunda halikuwapa ujuzi mpya. Matendo yao ya kutomtii na kutomwamini Mungu ndiyo yalikuwa “ujuzi mpya”. Kitendo hicho kilivunja uhusiano wao na Mungu na kikaweka uhusiano wao na Shetani. Maarifa yote mabaya na ya kutisha ndiyo yaliyofuatia).

1. Hili linapendekeza nini juu ya asili ya dhambi? (Ni kutokuamini na kutokutii kwa sababu tunafikiri ya kwamba tunajua zaidi ya Mungu).

C. Soma Warumi 5:16-17. Matokea ya dhambi ya Adamu na Hawa yalikuwa yapi? (Yalituletea laana/hatia).

1. Kwa nini? (Uhusiano wa mwanadanu na Mungu mkamilifu ulivunjika. Tukawa wadhambi ambao tukaupa utii wetu kwa Shetani).

2. Je, zawadi ya Yesu inatofautianaje na zawadi ya Adamu na Hawa? (Dhambi moja ilileta mpasuko kwenye uhusiano wetu na Mungu na kutuletea laana/hatia. Lakini, maisha, kifo na ufufuo wa Yesu kwa niaba/ajili yetu imefunika dhambi zote zilizofanyika tangu wakati wa Hawa).

D. Soma Warumi 6:11-13. Twajihesabuje kuwa “wafu” kwa dhambi? Je, hilo ni kama vile kurudia jambo la ujuzi wa mabaya? (Adamu na Hawa, kama wangetii, hatimaye wangeelewa kuhusu uovu-walakini wasingekuwa sehemu ya uovu huo. Tunaelewa kuhusu uovu kwa sababu ya Adamu na Hawa (pamoja na maanguko yetu wenyewe), lakini Mungu anatutaka tuishi kana kwamba hatujui uovu. Anatutaka tuwe “wafu” kwa ujuzi huo).


III. Dhambi: Mwanzo Wake Ndani Yetu

A. Je, tunaishije maisha ya kuifia dhambi?

B. Nilimpa Hawa wakati mgumu kwa kusema kuwa “Usiguse” pale ambapo huenda alikuwa anajaribu kuepuka dhambi. Unadhani ni nini ambacho kingekuwa njia salama zaidi kuepuka dhambi ya kula tunda lililokatazwa?

C. Soma Warumi 8:5-8 and Mathayo 5:27-28. Hebu tuangalie hili fungu la pili kidogo. Yesu anaonekana kusema kuwa kuna tatizo kwenye “kuzini nafsini?” Kwa nini hivyo? (Una nia ya kufanya uzinzi, kinachokosekana ni fursa tu. Kama ungekuwa na fursa, ungefanya uzinzi).

1. Je, fungu hilo la Warumi 8 linapendekeza nini kuhusu uhusiano uliopo kati ya akili zetu/mawazo yetu na dhambi? (Linapendekeza kuwa tunaanza na hatua ya kufikiri akilini kabla ya hatua ya kutenda kivitendo. Kile tunachokitenda huagizwa na kile tunachokifikiri. Aidha tutaangalia kile ambacho Mungu anakitaka au tutaangalia matamanio yetu ya kibinafsi).
a. Je, wazo hili “lafananaje” na hali ya Hawa? (Aliamua kutomtii Mungu kabla hajala tunda. Aliamua kutizama matamanio yake ya kichoyo. Paulo anapotuambia kuwa “tufe” kwa dhambi, anamaanisha kuwa tusiishi vivyo katika mawazo yetu. Tusitizamie matamanio yetu ya kibinafsi.

2. Je, unafikiria juu ya dhambi ambazo huzitendi?

a.Kama ndivyo, je, ni kama tu suala la muda kabla hujazitenda?

D. Rafiki, naamini dhambi kwa zaidi ni mtizamo-mtizamo wa ubinafsi. “ujuzi” wa uovu ulikuwa awali ya yote uamuzi wa kutomwamini na kutomtii Mungu. Yesu amekarabati uharibifu uliofanywa na Adamu na Hawa, ila naamini Paulo na Hawa wanatufundisha kuwa uaminifu na utii ni muhimu sana kwenye uhusiano wetu na Mungu. Je, utatubu dhambi zako na kumwomba Mungu kukupatia mtizamo wa uaminifu na utii?


IV. Wiki Ijayo: Neema.

Imetafsiriwa na kuandaliwa na
Mgune Masatu.

Monday, May 4, 2009

The Samoan singing Group



Hawa jamaa wanavaa kwao wanavaa sketi!!