Friday, May 22, 2009

SOMO LA TISA: MBINGUNI

(2 Wafalme 2 & 13, Mathayo 17, Ufunuo wa Yohana 21)
Maisha ya Mkristo: Somo la 9
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sememu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani, Kihispania, Kizulu, nk.


Utangulizi: Nini kinachokutia hamasa maishani? Pesa, heshima, nguvu/uwezo, upendo. mafanikio, Mungu au yote hayo? Kwa nini nimeorodhesha Mungu kati ya vitia hamasa vya mwanadamu? Kwa sababu Mungu yupo katika mchakato wa uhamasishaji. Kihamasisho kimoja kikubwa ni ahadi yake ya mbingu kwa wale walio waaminifu. Wiki iliyopita nilikuambia utafakari juu ya mkakati wa Shetani pale inapokuja kuhafifisha/kudhoofisha mamlaka ya Mungu. Unadhani ni nini mkakati wa Shetani pale linapokuja suala la mbinguni? Kama mbingu haipo, dhambi (ambayo ipo) inaonekana kuwa nzuri sana, si ndiyo? Angalau mwanzoni. Hebu tujivinjari ndani ya Biblia na kuona kile inachosema kuhusu ujira wetu wa milele!

I. Eliya, Elisha na Mbingu

A. Soma 2 Wafalme 2:1 na 2 Wafalme 2:11-12. Elia alikufaje? (Hakufa!)

1. Alikwenda wapi? (Alikwenda mbinguni moja kwa moja.)

2. Tunajifunza nini kuhusu mbingu kutoka kwenye haya mafungu machache? (Ni “juu” na ina usafiri wa umma (wa watu wote). Kwa dhati zaidi, lazima iwe sehemu halisi ambapo miili ya kawaida inaishi.)

3. Unaelezeaje mwitikio wa Elisha? Kurarua mavazi yako inamaanisha kuwa huna furaha. (Elisha alimwita Eliya “gari la Israeli na wapanda farasi wake.” Israeli haikuwa na magari na wapanda farasi. Elisha alikuwa anasema kuwa Eliya alikuwa nguvu ya Israeli, na alisikitika kumwona akienda.)

B. Soma 2 Wafalme 13:21. Nini kilitokea kwa Elisha pale alipokufa? Je, alifuata nyazo za rafiki yake Eliya? (Hapana. Mifupa yake ilikuwa kaburini.)

1. Je, hii inamaanisha kuwa Elisha hakuwa mbinguni? (Tunajua kwa hakika kwamba, tofauti na Eliya, mwili wake haukuwa mbinguni.)

II. Musa na Mbingu

A. Soma Kumbukumbu la Torati 34:5-7. Nini kilitokea kwa mtu muhimu Musa pale alipokufa? (Mungu alimzika!)

1. Je, Musa alikuwa mbinguni pale alipokufa? (Eliya anatuonyesha kuwa Mungu alikuwa na uchaguzi wa kumpeleka mbinguni, lakini fungu linasema kuwa badala yake Mungu alimzika.)

B. Soma Yuda 1:9. Yuda anaongelea juu ya nini? (Inavyoonekana, baada ya Musa kufariki, Mungu na Shetani walikuwa na malumbano/mgogoro juu ya mwili wa Musa. Katika malumbano hayo, Mungu alimkemea Shetani.)

1. Unafikiri kuwa ni nini kilikuwa kiini cha malumbano/mgogoro? (Bila shaka Mungu aliutaka mwili wa Musa na Shetani hakufikiri kuwa Mungu alikuwa na haki kwa mwili huo kwa sababu Shetani alikuwa “mtawala” wa dunia.)

C. Soma Mathayo 17:1-3. Nani aliyeshinda malumbano/mgogoro juu ya mwili wa Musa? (Mungu alishinda!)

1. Mungu aliupeleka mwili wa Musa wapi? (Lazima itakuwa mbinguni kwa sababu huko ndiko Eliya alikopelekwa!)

2. Mpangilio wa muda wa Musa kwenda mbinguni ulikuwa upi? (Muda fulani baada ya Mungu kuwa amemzika.)

III. Yesu Mbinguni

A. Soma Mathayo 22:23-28. Kwa nini Masadukayo waulize swali hili ikiwa hawakuamini katika ufufuo wa wafu? (Walitaka kuonyesha kuwa hilo lilikuwa wazo lisilokuwa la kivitendo.)

B. Soma Mathayo 22:29-32. Yesu anasema nini kuhusu kama ufufuo uko mbeleni mwako? Yesu anasema nini kuhusu mipango ya Mungu kwa waaminio? (Yesu kwa hakika anaidhinisha wazo la kwamba tutafufuliwa. Analijenga hilo katika Biblia na katika uwezo wa Mungu.)

C. Tunaona kutoka kwenye visa hivi na tamko la Yesu kwamba kuna mbingu na pia kuna ufufuo ujao. Hilo linatufundisha nini kuhusu upendeleo alio nao Mungu ndani yako? (Kwamba Mungu ana mpango wa wokovu kwetu ili kwamba kama tu waaminifu, tunaweza kuishi pamoja naye.)

IV. Lini Mbingu?

A. Kuna uvumi mkubwa na mjadala kuwa nini kinatokea pale mtu anayeamini anapokufa. Wengine wanaamini kuwa “roho” ya mtu inakwenda mbinguni wakati mwili unaoza. Wengine wanaamini kwamba roho haipo tofauti na mwili, na mwili na roho vinakuwa katika hali ya kutokuwa na fahamu kaburini hadi ufufuo. Je, visa vya Eliya, Elisha na Musa vinatufundisha nini kwa hali ya juu kabisa ya uhakika? (Eliya anatufundisha kuwa Mungu anaweza kutuchukua mbinguni moja kwa moja bila kuonja mauti. Elisha anatufundisha kuwa hali ya kawaida ya kifo ni kwamba miili yetu inaoza na kubakia hapa duniani. Musa anatufundisha kuwa mara baada ya kufa, na miili yetu kuzikwa, Yesu anaweza kutufufua na kuturejesha maishani kabla ya ufufuo wa jumla.)

1. Visa hivi vinaelekea kutufundisha nini kuhusu kuwa na roho yenye utambuzi inayojitegemea? (Wana tabia ya kubainisha uongo. Kwa nini mwili wa Eliya ulichukuliwa juu? Kwa nini mwili wa Musa uwe kiini cha mpambano kama tuna roho iliyopo mbinguni? Ukweli kwamba Mungu alikusanya miili ya waaminio maarufu wawili yaelekea kuonyesha kwamba mbinguni tutakuwa na miili yetu. Mungu anaweza kutuchukua mbinguni wakati wowote kipindi cha uhai wetu au baada ya kuwa tumefariki. Lakini, inaonekana kuwa anachukua kila kitu, na anavichukua mbinguni, mahala ambapo miili inaonekana kuwa ya muhimu.)

V. Wewe na Mbingu

A. Kwa hiyo, upo mbinguni na mwili wako wote. Kuna nini pale cha kufanya? Je, kuna sehemu ya maji? Kuna miti ya kukwea? Je, ni nini kuhusu mikahawa mizuri?

B. Soma Ufunuo 21:2-3. Kitu cha kwanza kufanya mbinguni ni nini? (Tutakuwa na uhusiano wa karibu na Mungu. Muumba wetu na Mkombozi wetu-yeye atupendaye upeo (zaidi ya tunavyoweza kufikiria)-atakuwepo.)

C. Soma Ufunuo 21:4. Hali ya hisia zetu itakuwaje mbinguni? (Hatutasikitika. Hapatakuwepo na mauti wala maumivu. “Mambo ya kwanza” kuelekea kaburini yamekwisha kupita.

D. Soma Ufunuo 21:5 na Isaya 65:17. Unapenda mambo mapya? (Yote yatakuwa mapya mbinguni na katika nchi mpya.)

E. Soma Ufunuo 21:10-11 na Ufunuo 21:18-21.
Fikiria kito kizuri sana na cha thamani. Halafu tafakari mji wote unaoonekana kama kito kimoja kikubwa kizuri cha ajabu! Hayo ndiyo maisha yetu ya baadaye!

1. Kwa nini Mungu afanye Yerusalemu mpya kama hivyo? (Muda wa kujitoa/kujikana nafsi umepita. Hii inapendekeza kwamba Mungu huumba na kutupatia dunia kwa ukarimu mkubwa.)

F. Soma Ufunuo 21:23-26. Tunajifunza nini kuhusu masharti ya mwangaza na mwelekeo wa ulalaji?

1. Majadiliano kuhusu “wafalme” na “mataifa” yanapendekeza nini? (Ya kwamba tutakuwa na mpangilio.)

G. Soma Ufunuo 22:1-3. Hili linatuambia nini kuhusu sehemu za maji, ukweaji miti na kula kule mbinguni? (Vyote hivyo vipo huko.)

1. Wazo la ulaji na unywaji huu unapendekeza nini kuhusu uwepo wa roho? (Ya kwamba sisi siyo roho.)

2. Ona tena rejeo la “mataifa.” Mjadala wa Yerusalemu mpya unajumuisha uhalisia wote wa mambo ambao u dhahiri kwetu-isipokuwa utadhihirishwa kwa uzuri zaidi ya tujuavyo. Hili linatufundisha nini kuhusu mbingu? (Ya kwamba itakuwa ya kawaida/yenye kujulikana/zoevu kwetu katika njia nyingi.

H. Ninasoma kitabu kilichoandikwa na Randy Alcorn kinachoitwa "Mbingu." Alcorn anaiangalia Biblia na kuhitimisha kwamba Mungu anapoileta Yerusalemu Mpya hapa duniani iliyofanywa upya, kwamba alama za kiujumla za kijiografia zitaumbwa upya. Ufunuo 21:1 inafunua kuwa bahari haipo tena. Hiyo itapanua ukubwa wa ardhi ya sasa. Kwa hiyo, uelewa wa Alcorn unakubalika. Ningependa kuendelea kuishi Virginia . Je, ungependa, katika nchi mpya, kuishi pale unapoishi kwa sasa? Kuweza kutembelea mahala pale ulipokulia?

I. Soma Yohana 14:2-3. Oh Hapana! Je, sasa tumepunguziwa hadi kubakiwa na “chumba” kule mbinguni? (Hapana. Hii ni “Yerusalemu Mpya” tunayoimiliki. Katika Yerusalemu Mpya kuna sehemu yenye ukomo. Tuna umiliki wetu katika Yerusalemu na nchi zetu za nyumbani popote pale tunapotaka.)

1. Soma Isaya 65:21-22. Je, hii ni nchi ya nyumbani ambayo nimeirejea hivi punde? (Sina hakika na jinsi ya kushughulika na hili fungu. Nafikiri kimsingi linarejea mpango wa Mungu kwa Wayahudi kama wangekuwa waaminifu kwake. Hata hivyo, jinsi baadhi ya unabii ulivyo na utimilizwaji zaidi ya mmoja, nadhani hili laweza kuwa sahihi kabisa (kwa kiwango fulani) kujielekeza mbinguni pia. Kwa hakika inatupatia mtazamo ambao Mungu anautaka kwa ajili yetu.)

J. Rafiki, ungependa kuishi milele katika sehemu nzuri na isiyo na kasoro? Sehemu ya furaha? Sehemu nzuri kupita kiasi? Mungu amewaahidi watu wake mbingu, Yerusalemu Mpya na nchi mpya. Waweza kuwepo. Utatubu dhambi zako kwa Mungu, kuyakubali maisha na kifo cha Yesu kwa niaba yako, na kumwomba Yesu kuungana naye katika ule ufufuo wenye utukufu katika maisha mapya pamoja naye?

VI. Wiki Ijayo: Uanafunzi.

No comments:

Post a Comment