Friday, May 29, 2009

Somo la 10: Uanafunzi

Uanafunzi
(1 Wakorintho 12, Kutoka 18, Mathayo 20, Marko 8)
Maisha ya Mkristo: Somo la 10
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sememu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani, Kihispania, Kizulu, nk.

Utangulizi: “Ongoza, fuata au pisha njia” ni msemo wenye sifa ya msingi ya Thomas Paine, “Baba wa Taifa” la Marekani. Kama ningekupa chaguo la hayo matatu, wangapi mngechagua “kufuata?” Nahisi siyo wengi. Wengi hupenda kuongoza ama kwenda njia zao wenyewe. Inamaanisha nini kuwa mfuasi wa Mungu? Je, hii ni aina ya kitamaduni ya mfuasi? Au je, huyu ni mfuasi ambaye pia anaongoza? Hebu tujivinjari katika Biblia na kubaini!

I. Mwili wa Wafuasi

A. Soma 1 Wakorintho 12:27. Je, kuwa sehemu ya mwili wa Kristo ina nini cha kufanya na dhana ya uanafunzi? (Tunapomfuata Yesu, tuna sehemu ya kufanya katika utendaji kazi. Cha kufurahisha zaidi, utendaji kazi wetu kama wanafunzi unalinganishwa na “mwili.”)

B. Soma 1 Wakorintho 12:28. Kati ya majukumu haya, ni yapi ni majukumu ya “kiuongozi” (“Mitume” na “maongozi” yanaonekana kama yanaongoza kiaina.)

1. Wafuasi ni wapi katika kundi hili? (Hilo siyo rahisi kulielezea, si ndiyo? Nadhani “wasaidizi” wanaweza kuwa wafuasi kwa muktadha fulani.)

2. Kwa nini suala la kiongozi na mfuasi ni gumu kulijibu? Kwa nini Mungu ashindwe kuliweka hili dhahiri?

3. Kwa nini Biblia inalinganisha kanisa na mwili badala ya jeshi au taifa? (Kwa sababu msitari kati ya mfuasi na kiongozi hauko wazi sana . Katika jeshi au taifa, kuna viongozi wachache na wengine wote waliosalia hufuata. Lakini, isipokuwa kwa ukweli kwamba Mungu ni kiongozi wetu, kanisa linaonekana kama kitu fulani tofauti kabisa. Nafikiri kwa hakika kabisa hii ndiyo sababu kwamba Mungu alitumia mfano wa mwili badala ya jeshi kuelezea kanisa lake.)

4. Soma 1 Wakorintho 12:20-21. Kanisa linafanyaje kazi pale linapokuja suala la viongozi na wafuasi? (Badala ya mpango wa kiongozi/mfuasi ulio wazi, tunaona juhudi zilizoratibiwa ambapo kila sehemu ni ya msingi. Kila mtu ni muhimu. Kila mtu ana sehemu kubwa sana . Thomas Paine, muasisi wa taifa la Marekani hakuwa na kanisa mawazoni mwake.)

II. Viongozi Wanaojifunza

A. Soma Kutoka 18:13. Je, watu walifurahia hali hii? (Walikuja kwa Musa. Hata hivyo, usemi kwamba “wakasimama kumzunguka….. tangu asubuhi hata jioni” unaweza kuakisi huduma ya polepole.)

1. Je, Musa alifurahia hali hii? (Kazi nzuri iliyoje zaidi ya kuzungumza kwa ajili ya Mungu! Hata hivyo, alifanya kazi kwa saa nyingi.)

B. Soma Kutoka 18:17. Je, haya ni maneno ambayo Musa alitarajia kuyasikia? Je, hakuwa akifanya jukumu kubwa kuzungumza kwa ajili ya Mungu na kulisaidia taifa lake?

C. Soma Kutoka 18:18-23. Je, kama ungekuwa Musa, ungeitikia vipi ushauri wa Yethro (baba mkwe wako)? Ukizingatia kwamba, wewe ndio uliongea na Mungu, na siyo yeye. Kwa nini umsikilize pale ambapo unanena kwa ajili ya Mungu?

1. Gundua (angalia) Kutoka 18:19. Je, Yethro anafafanua kazi ya Musa? (Ndiyo. Anasema kwamba jukumu la Musa lapaswa kuwa kwenda kwa Mungu kwa ajili ya watu, siyo kumuamulia Mungu. Hili ni sahihisho lenye akili. Hii inaashiria kwamba Musa anaelekea kuamini kupita kiasi katika umuhimu wake mwenyewe, wakati ambapo watu wengine wanaweza kufanya kile ambacho Musa anakifanya.)

2. Gundua (angalia) Kutoka 18:23. Je, Yethro anasema nini? (Anasema kwamba Mungu anahitaji kuthibitisha ushauri wake.)

3. Hadi sasa tunajifunza nini kuhusu uanafunzi katika kisa hiki? (Huu ni mfano mwingine wa sheria ya “mwili” ya uongozi-kwamba badala ya kufanya kazi peke yake, Musa anahitaji kuwategemea watu wengine kumsaidia katika jukumu hili muhimu. Jukumu muhimu linahitajika kusambazwa kwa watu wengine wenye uewezo.)

D. Soma Kutoka 18:24-26. Ni kitu gani kizuri tunachojifunza kutoka kwa Musa kama kiongozi? (Kwamba ingawaje anaonekana kupitiwa kidogo na umuhimu-binafsi, anafuata ushauri. Anaonyesha unyenyekevu katika ukubali na utekelezaji wa ushauri mzuri aliopewa.)

1. Hili linatufundisha nini kuhusu taasisi? (Kuendesha taasisi kwa usahihi kunahitaji mpangilio/maandalizi. Kugawanya majukumu, kuchagua watu hodari/wenye ujuzi, na kumuweka Mungu kama kiongozi wa programu ndio ufunguo.)

III. Viongozi Watumishi

A. Soma Mathayo 20:20-21. Kwa kusoma haya mafungu mawili, unafikiri jibu lapaswa kuwa lipi? (Ni aina gani ya viongozi wajao hutuma “mama” kuwafanyia kazi zao za muhimu sana?)

B. Soma Mathayo 20:22. Je, mama ni msanii (mwenye kutoa sauti kana kwamba imetoka kwa mwingine)? Je, hili jibu la “twaweza” ni nini? (Si tu kwamba wanawe wanamtuma mama, bali wanasimama pembeni na kusikiliza mazungumzo!)

1. Unafikiria nini juu ya jibu la wanawe? (Yesu aliwaambia kwamba hawajui kile wanachokiomba, na wao (wangali wakiwa katika dimbwi la upumbavu) wanajibu kuwa “Twaweza.” Viongozi wakamilifu-wadhaifu na mabubu kiasi cha kutosikia!)

C. Soma Mathayo 20:23. Ni nani anayeamua katika uongozi wa kanisa? (Mungu. Yesu anatoa jibu la upole, lakini anaweka wazi kuwa Mungu Baba ndiye atakayefanya maamuzi haya.)

D. Soma Mathayo 20:24. Kwa nini hawakuwa na furaha? Kwa sababu mama zao hawakuwa wenye hamasa vya kutosha? Kwa sababu hawakufikiria kuuliza kwanza? Kwa sababu hawataki kufuata, wanataka kuongoza?

E. Soma Mathayo 20:25-28. Je, Yesu anahitaji mfuasi/kiongozi wa aina gani? (Kiongozi mtumishi. Dhana ya ajabu kiasi gani: kiongozi ambaye anatumia mamlaka kuwasaidia watu wengine, na siyo kujisaidia yeye mwenyewe.)

1. Maneno haya ni yenye mhimili katika historia ya dunia ya sasa. Wanazuoni/watafakari wa siasa wa hali ya juu wa kale Plato na Aristotle,walikuwa na wazo hili kwamba kulikuwa na watu wachache wa hali ya juu ambao wanapaswa kuwa viongozi na wengine waliobaki wanapaswa kuwatumikia kwa ajili ya manufaa mazuri. Yesu anasema kwamba viongozi wanapaswa kuwatumikia watu wao. (“Mtu yeyote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu.”) Ni kutoka katika fundisho hili kwamba tunapata wazo la “mtumishi wa umma” ambalo ni mhimili katika demokrasia ya Marekani.)

2. Somo letu siyo juu ya serikali isiyokuwa na uhusiano wa kidini. Ni nini somo kwa ajili ya uongozi wa kanisa leo?

a. Ni somo gani kwa ajili yako?

IV. Uanafunzi

A. Soma Marko 8:34-38. Je, inamaanisha nini kujitwika msalaba wetu?

1. Soma Mathayo 11:28-30. Nafikiri “nira” ya Yesu kimsingi ni sawa na “msalaba” wake. Inawezaje kuwa “nyepesi” pale ambapo inaonekana kuwa ngumu na ya kutisha/kuogofya? (Kutumikia matakwa yako peke yako inachosha (inaleta uchushaji). Kuwatumikia wengine hufanya maisha kuwa yenye manufaa na yaliyobarikiwa. Inaonekana kana kwamba ni vya kutisha sana kujitoa maisha yetu, lakini Mungu si kwamba anatupatia uzima wa milele kwa mbadilishano huo (mbadilishano mzuri!), bali husaidia wengine katika kuifanya nira “laini”.)

B. Soma Mathayo 7:21. Umewahi kusikia usemi “fimbo kubwa, pasipo ng’ombe?” Unadhani inamaanisha nini? (Mtu anayecheza sehemu ya kuwa mchunga ng’ombe, lakini asiye na ng’ombe-hana kitu.)

1. Je, hicho ndicho Yesu anachokimaanisha hapa? (Inaonekana kwamba Yesu anasema kuwa watu hawa wanaongea tu, hawatendi.)

C. Soma Mathayo 7:22-23. Hebu subiri kidogo, watu hawa wana matendo mengi. Unawezaje kuelezea kwamba Yesu anawakataa wakati wana matendo? (Cha msingi ni kwamba Yesu anasema “ Sikuwajua kamwe.” Mapenzi ya Mungu Baba ni kwamba tumjue Yesu. Hii ndio kazi ya msingi ya mwanafunzi. Kama hatumjui Yesu, basi kazi zetu zimeelekezwa pasipostahili.)

D. Rafiki, je, hii iinakupa picha ya kutosha ya uanafunzi? Mwanafunzi wa kweli anamjua Mungu na pale anapofaa katika kazi ya kanisa. Mwanafunzi wa kweli ana lengo la kusaidia-siyo lengo la kujitukuza nafsi. Kama mtizamo wako si sahihi, je, utamwomba Roho Mtakatifu kuubadilisha leo? Kama haulitumikii kanisa kwa namna fulani, je, utamwomba Mungu kwamba akuonyeshe namna ya kutumikia?

V. Wiki Ijayo: Uwakili.

Imetafsiriwa na kuandaliwa na,
Mgune Masatu.

No comments:

Post a Comment